Kuna jambo gumu linalonipa uchungu moyoni

By Godfrey Mushi , Nipashe Jumapili
Published at 04:52 PM Mar 24 2024
Askofu wa Dayosisi ya Kaskazini ya Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dk. Fredrick Shoo.
PICHA: KKKT
Askofu wa Dayosisi ya Kaskazini ya Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dk. Fredrick Shoo.

HOJA ya Askofu wa Dayosisi ya Kaskazini ya Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dk. Fredrick Shoo, kuja na mbinu mpya za kuzuia upigaji kanisani, imenikosha na inanitia moyo.

Askofu Dk. Shoo ana jicho la tatu lisilo la kawaida. Jicho hilo ukilifungua utaona vitu vingi ambavyo wenzio hawaoni.

Jicho hilo likifunguka huwa halizibwi na kitu chochote, hata iwe kiza kinene mbele yako, utaona kama mtu aliyekuwa juani mchana. Ni jicho linalokupeleka kwenye maisha ya watu, utawajua watu majina na maisha yao; hata kama hawajakwambia.

Kauli ya Askofu Dk. Shoo kuhusu matumizi ya fedha mbichi kanisani, inatoa tafakuri ya kina kuhusu aina hiyo mpya ya uipigaji.

Amesema maneno yanayopasua ngoma za masikio yetu. Uwazi katika jambo kama hili, ni darasa tosha ambalo kila mmoja wetu anapaswa kujifunza.

Hakuna ubishi kwamba kwa kauli yake anaona kuna mwanya mkubwa wa upotevu wa fedha ndiyo maana anataka jicho kali zaidi liwekwe kungalia fedha mbichi zinazotumika bila kupelekwa benki.

Kwa jicho lake katika matumizi ya pesa mbichi, uko ulazima kama kiongozi mwenywe maono, kuhakikisha malipo yote yanayofanywa na sharika zote, yanapelekwa benki siku hiyo hiyo.

Ili kuepuka matumizi ya pesa mbichi kanisani, iwake, inyeshe, mapato yote yasibakie mikononi mwa wachache, hasa Wachungaji ili kuepusha matumizi ya pesa mbichi.

Iko haja ya kufuatilia na kuhakiki hati zote za malipo, zinakuwa viambatisho wakati wote, na isiwe tu mpaka wakati wa ukaguzi.

Kuwapo na vitabu vya kumbukumbu vinavyoonyesha kiasi cha fedha zinazopatikana kupitia vyanzo vyake mbalimbali, ikiwamo sadaka.

Mwanzoni mwa wiki hii, katika kikao chake na zaidi ya Wachungaji 300 wa Dayosisi hiyo, Dk. Shoo alieleza kile asichokubaliana nacho na akitaka kuepukwa huku akionya fedha za sharika zisitumike ndivyo sivyo, huku akihadharisha Wachungaji wasikubali kuruhusu matumizi ya pesa mbichi ambazo hazijapita kwenye vitabu.

Dayosisi ya Kaskazini ya KKKT, inaundwa na majimbo matano ya Kilimanjaro Mashariki, Kilimanjaro Kati, Hai, Siha na Karatu.

Askofu Dk. Shoo, ambaye amekuwa Mkuu wa Kanisa la KKKT kwa miaka minane, alikemea matumizi ya fedha mbichi kanisani wakati wa kikao kazi kilicholenga pamoja na mambo mengine, kuwakumbusha Wachungaji kuwa waadilifu katika masuala ya fedha, kazi na mienendo ya maisha.

Katika nasaha zake, Dk. Shoo alionya akisema kuna taarifa za fedha za Usharika kutumika ovyo, akibainisha wako baadhi ya Wachungaji wanatumia nafasi zao kushawishi watu wasiokuwa waadilifu na wasiojua wajibu wao katika Baraza la Usharika.

“Unakuta Mchungaji anasema, hebu nipe 100,000 hapo, pesa ambayo ni mbichi haijapita kwenye vitabu. Unapofanya hivyo, ni kukosa uaminifu na unafundisha wewe wale wengine. Hii haina baraka, taratibu za utunzaji fedha zifuatwe,” alinukuliwa akiyasema hayo.

Aidha, Askofu Dk. Shoo aliwasihi Wachungaji hao kuendelea kutunza maadili ya utumishi.

 “Ndugu zangu Wachungaji, tumeitiwa huduma hii takatifu kwa neema ya Mungu. Ninawakumbusha na kuwasihi sana, tutunze maadili ya utumishi na haya yanaanzia na wewe mwenyewe unavyoonekana. 

How you behave (mwonekano wako ulivyo), usionekane kama Mchungaji wa kijiweni au mtu wa kijiweni, tafadhali! utumishi huu una heshima yake, maneno yako unayozungumza yatofautiane na maneno ya kijiweni; lakini tutunze maadili ya wito wetu,” alisisitiza.

Kwenye hotuba yake, Askofu Dk. Shoo, aliwataka Wachungaji kuwa waadilifu katika masuala ya fedha na kuweka kumbukumbu za fedha kwa uadilifu na kufuata taratibu.

Uchungu ni hisia abebazo mtu baada ya kufikwa na jambo au maudhi fulani. Ni mwitikio wa kihisia uliosababishwa na tukio lililo mkosesha mtu amani moyoni.

Labda hujanielewa. Uchungu  ni ishara ya awali kwamba kuna jambo lililosababisha uchungu moyoni, ambao imeshindikana kuachiria.

Katika Kitabu cha Isaya 38:15 imeandikwa. Niseme nini? Yeye amenena nami, na yeye mwenyewe ametenda hayo; Nitakwenda pole pole miaka yangu yote, kwa sababu ya uchungu wa nafsi yangu.

·         Godfrey Mushi ni Mwandishi Mwandamizi wa Nipashe, Kanda ya Kaskazini. Anapatikana kwa barua pepe: [email protected] na Simu ya mkononi: +255 715 545 490