CHADEMA inavyoharibu mipango mizuri ya Rais Samia

By Nipashe Jumapili
Published at 02:10 PM Jan 21 2024
PICHA:
Na Mtandao
PICHA:

WAZIGUA wana msemo maarufu usemao ‘Tindi dyahoswa nchereko’ wakimaanisha kuwa siku zote mgomba unaponzwa na uzazi. Mgomba ukikomaa na kubeba mkungu wa ndizi, maisha yake yanakoma.

Mgomba unaokatwa baada ya kuzaa, huwa pembeni yake umechipua mwingine. Msemo wa kabila hili lenye asili Handeni mkoani Tanga, una maana kubwa. Umebeba ujumbe mpana. Hata kwenye ulingo wa kisiasa unajitokeza na kueleweka.

Unashabihiana pia hata kwa kuangalia mfumo na aina ya uongozi anaojaribu kuutumia katika madaraka yake Rais Dk. Samia Suluhu Hassan.

Mgomba kama mmea hauhisi maumivu hata pale unapokatwa. Si kwa binadamu kama Dk. Samia. Huumia anapoona dhamira njema aliyo nayo inashindwa kueleweka lakini kutokana na mamlaka makubwa aliyo nayo na anavyojitoa akiheshimu kila kundi ndani ya nchi,  hakika alistahili uungwaji mkono kuliko ilivyo sasa.

Watu wanaojitokeza kulaumu, kushutumu na kukejeli huku wakiwa ni viongozi wa kisiasa kama ilivyo kwa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), wanaendana na msemo kuhusu mgomba. Ingawa ni Rais wa nchi, lakini aina ya uongozi wake akiwa mama anayelea makundi yenye tabia tofauti, bado anaponzwa na uzazi wake.

Pengine asingekubali kuwa kiongozi, asingeghadhibika na karaha zinazofanywa kwa makusudi kutoka kwa watu ambao wengine amewasaidia kuendelea na siasa zao tofauti na ilivyokuwa katika uongozi wa awamu ya tano chini ya Hayati Dk. John Magufuli.

Wiki iliyopita, Mwenyekiti wa CHADEMA, Freeman Mbowe, alitangaza maandamano aliyoita ya amani. Maandamano hayo alisema yatafanyika Januari 24, mwaka huu,  kushinikiza serikali iondoe bungeni Miswada ya Sheria za Uchaguzi.

Kauli hiyo imekuja wakati Kamati ya Bunge ya Utawala, Katiba na Sheria ikikamilisha sheria iliyosomwa bungeni Novemba 23, 2023 mjini Dodoma. Miswada hiyo ni Sheria ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani wa Mwaka 2023;  Sheria ya Tume ya Uchaguzi wa Mwaka 2023 na wa Mabadiliko ya Sheria ya Vyama vya Siasa wa mwaka 2023.

Kabla ya miswada hiyo kufikishwa bungeni kwa utaratibu wa kawaida, watu mbalimbali wakiwamo viongozi wa vyama vya siasa walitoa maoni yao. Kwa sababu hii tu, CHADEMA wakiongozwa na mwenyekiti wao, wanaonyesha wanavyojaribu kutafuta njia ya kupandikiza chuki kwa jamii.

Mkutano Maalum wa Baraza la Vyama vya Siasa uliofanyika Dar es Salaam Septemba 11 hadi 13, mwaka jana, na kushirikisha zaidi ya 500 wakiwemo viongozi mbalimbali wa kisiasa, uliokuwa na  nia nzuri ya kujenga msingi wa haki na demokrasia ya vyama vingi vya siasa. 

Mkutano huo haukuwa wa kwanza kwa kuwa awali ulifanyika jijini Dodoma kuanzia Desemba 15 hadi 17, 2021 na kuhudhuriwa na Rais Samia. Ni mkutano huo uliofanikisha kuundwa kwa kikosi kazi.

Pamoja na dhamira njema ya serikali, bado kuna watu wanaohamasisha maandamano wakisema ni ya amani! Hizi ni dalili kwamba CHADEMA wana kiu na shauku ya kurudisha nyuma nchi katika wakati huu ambayo kipaumbele ni uchumi kikishika hatamu. 

Hakuna maandamano ya amani yasiyo na kibali. Kwa bahati mbaya, ili maandamano yapate kibali cha polisi, ni sharti wanahitaji pia sababu madhubuti ya kuandaliwa kwayo.

Kwa sasasababu haipo. CHADEMA wanasema wanashinikiza serikali iondoe miswada ya uchaguzi bungeni. Wanasahau ilipitia katika hatua zote zikiwamo za maoni ya Watanzania. Kama kweli itaondolewa bungeni, nuia njem,a ya Rais Samia ya kudumisha demokrasia na utawala bora itakuwa bure.

Ilishawahi kutokea kasumba kama hii wakati wa Awamu ya Nne, chini ya Rais Jakaya o Kikwete, uamuzi wa kusitisha mchakato wa Katiba Mpya ulifanywa baada ya chama hiki kususia hatua za mwisho.

Kulizuka mivutano kati ya serikali na CHADEMA. Kelele, malalamiko, shutuma na wakati mwingine kukejeliana hata kwa watu wenye heshima kukasababisha mchakato kuzimwa na serikali.

Shauku nyingine ya CHADEMA ni kutaka mchakato wa Katiba mpya uibuliwe. Bahati nzuri serikali ilishaweka hadharani hatua zitakazofanikisha ujio wa Katiba Mpya.

Kwa Tanzania inayoendesha siasa za vyama vingi,  si jambo la manufaa kusikiliza mtazamo wa chama kimoja. Inafaa watu kukaa na kujadiliana pindi kunapoibuka mkivutano na hivyo  ndivyo anavyopenda pia Rais Samia.

Kwa mtazamo wa CHADEMA, lengo lao ni kuivuruga amani ya nchi kwa faida zao binafsi. Wanafanya chokochoko ili serikali ivurugike wakiamini watanufaika. Kama hivi ndivyo wanavyowaza, ni wazi wanajidanganya. Ni vyema wakasukuma ajenda ya maeridhiano kwa njia ya vikao na wasijione wakubwa kuliko vyama vingine vya siasa. 

Malengo yao, kwa bahato mabaya.  hayawezi kufanikishwa kwa kuhatarisha usalama wa nchi . CHADEMA haina nguvu na upekee kuliko vyama vingine vya siasa. Kujiona wao wana uwezo wa kufanya lolote watakalo ni sahihi.

Vyama viheshimiane ili nao waheshimike mbele ya hadhira na hili likifanyika,  nchi  itaenda vizuri na kudumisha msamiati wa Tanzania kisiwa cha amani. Kuonyesha  ubabe mbele ya mamlaka ni hatari kubwa na haya yamewahi kutokea miaka kadhaa iliyopita na kuathiri nguvu kazi ya taifa. 

Ni kweli Katiba inaruhusu maandamano kama ilivyotajwa kwenye Ibara ya 20(1) lakini Sheria ya Polisi 43 (1) inataka watu watoe taarifa saa 48 kabla ya maandamano  kuanza. 

Katika sheria hiyo pia imewekwa wazi kuwa polisi wanaweza kuruhusu au kuzuia kufanyika kwa maandamano hayo kwa kuangalia hoja zao kama chombo cha ulinzi na usalama.

Wanaweza kusema wana uhaba wa polisi, majanga, ujio wa viongozi wajuu wa kitaifa nk. Na kwakuwa wao ndio wenye dhima ya ulinzi, itakuwa si jambo zuri kutokea mtu au kikundi cha watu kupinga hoja walizopewa na polisi.

Kama kikundi cha watu kitakaidi maelekezo halali ya wanaohusika na ulinzi wa watu na mali zao, si vibaya kama watatumia nguvu bila kuangalia madhara yanayoweza kutokea. Mwarobaini wa jambo hili ni watu kufuata sheria. Hakuna maandamano ya amani yasiyo na kibali cha polisi. 

Hii ndiyo sababu madhubuti ya watu kuomba ulinzi pindi jamii inapohitaji maandamano. CHADEMA wanajua hili, ila wanalipuuza kwa sababu dhamira yao si kuandamana ili kushinikiza hoja zao zisikilizwe, ila kutafuta vurugu ili kuitusi serikali mbele ya marafiki zao wanaodhamini utendaji wa chama chao.

Huu ndio ukweli ambao Watanzania wote wanapaswa kuufahamu. Bahati mbaya wanafanya haya mbele ya Rais ambaye amekuwa rafiki na kipenzi cha demokrasia. Rais anayetaka watu wafanye siasa bila kuingiliwa. Rais anayetafuta namna nzuri ya kudumisha umoja, mshikamano, ushirikiano na maridhiano ya kisiasa. 

0712053949