Siri pekee ya mafanikio kimaisha ni hii

By Pascal Mayala , Nipashe Jumapili
Published at 09:49 AM Jun 09 2024
Jedwali la mafanikio.
Picha: Mtandao
Jedwali la mafanikio.

LENGO la vyombo vya habari ni kuihudumia jamii. Ukikutana na jambo fulani zuri, linaloweza kuisaidia jamii, unaliandika ili kushirikisha wengine. Leo nawaletea mada ngumu kidogo ya jambo linalohusu kupata mafanikio kwa kutumia kitu kinachoitwa ‘manifestation’.

Kabla sijaendelea, naomba kutoa angalizo kwamba mada hii haina uhusiano na imani ya dini yoyote bali ni kwa ajili ya watu ambao ‘open minded’. Hawa ni wale wanaofikiria wenyewe na kwa kina. Mtu wa aina hiyo akiambiwa jambo lolote, kabla ya kuliamini, analifikiria kwanza kisha kulikubali na kuliamini. Kinyume cha watu wa kundi hilo, wako watu ambao ni ‘close minded’, wale ambao wakiambiwa jambo, wanaamini moja moja na hawahitaji kufikiria. 

Kwa mantiki hiyo, mada hii ni ya watu wanaofikiria lakini wale waliofikirishwa na kuziamini dini zao, hapa sii mahala pao. Nasema hivyo ili tusije kuleta mabishano ya imani za dini. Soma andiko hili huku umeshikilia imani ya dini yako. 

‘Manifestation’ ni kulidhamiria jambo kwa dhati ya moyo wako. Dhati hiyo  ya dhamira yako na juhudi yako kulifanikisha, inazifungua nguvu zilizoko ndani yako na kulitimiza jambo lako na linakuwa. 

Somo hili kama lilivyoandikwa na mwandishi Ingrid Clarke katika kitabu cha ‘Seven  Pillars of Manifestations’, lina nguzo saba ambazo ni Msingi wa ‘Manifestation’,  ‘Sheria za Manifestation’, Mitetemo ya ‘Manifestation’, Kuweka Nia, kuona kwa jicho la ndani, Kukuamini ni kweli, na mchakato wa utekelezaji wake.  

Kwanza kabisa tujiulize ‘manifestation’ ni nini? Katika andiko langu kuhusu ‘psychic powers’, nilisema kitu chenye nguvu sana katika mwili wa mwanadamu ni nia (will power). Wazungu  wanasema “where there is a will, there is a way”, msemo huu hata waswahili tunao, unaosema, “penye nia, pana njia”. 

Manifestation ni kitendo cha kutumia mawazo yako, kufungua milango ya nguvu zilizo ndani yako, kufanikisha mambo yako. 

Dini zote zinatufundisha tumeumbwa na Mungu na kuelezwa huyo Mungu yuko juu mbinguni, peponi au ahera, hivyo ukifa bila dhambi utaingia mbinguni na kumwona Mungu. Ukifa na dhambi, tunaamini kwamba utakwenda motoni kwa shetani kwenye jehanamu a moto wa milele. Kwa hiyo wengi wakisali wanatazama juu wakijua ni kweli Mungu yuko juu mbinguni kule mawinguni. 

Ukweli ni kuwa mbinguni na motoni ni hapa hapa duniani. Kuna ulimwengu wa aina mbili, ulimwengu wa mwili  na ulimwengu wa roho.  

Mungu alimwumba binadamu kwa kufinyanga udongo, kisha akampulizia pumzi ya uhai, hivyo mwili wa binadamu una sehemu mbili, yaani mwili wa nyama na mwili wa roho.  Mtu anapokufa, japo wanaita amekata roho, kinachokufa ni mwili wa nyama tu ambao unazikwa na kurejea kuwa mavumbi lakini roho inatoka, na kurejea kwake. Ndiyo mana kuna maneno yaliyozoeleka kwamba “sote ni wa Mungu na kwake tutarejea.” 

Hata ile siku ya mwisho ya ufufuko wa miili, miili inayofufuliwa ni  ya roho. Hii  miili ya nyama, mtu akifa ndiyo mwisho wake, hivyo wanaochoma, wako sahihi na wanaozika kwa heshima zote kwa masanduku ya gharama na kujengea makaburi, ni kujifurahisha tu nafsi zao. Mtu  akiisha kufa, ile mwili hauna maana tena.  

Sasa ile pumzi, roho ambayo Mungu amempulizia binadamu ni roho ya Mungu, hivyo kila binadamu anao u- Mungu ndani yake. Ile dhana kuwa Mungu yuko mbinguni ameketi kwenye kiti cha enzi, ni kweli lakini pia Mungu yuko ndani yako, kupitia roho yake, na hii ni ile kanuni ya uwapo wa Mungu ndani yako.  

Kwa mantiki hiyo, ‘manifestation’ ni kitendo cha kumtumia Mungu aliyeko ndani yako, kumtuma akunyooshe mambo yako. Kwa mantiki hiyo,  binadamu tuna nguvu za kufanya mambo mengi, lakini wengi hawajijui kama wanazo. Wale wahubiri wa miujiza ya uponyaji, wanatumia uwezo wao kukumanifestia. Kinachokufanya  ni imani yako na nguvu zilizo ndani yako na si nguvu za muhubiri. 

Kwa vile tumepewa nguvu hizi bure, kuzitumia pia ni bure. Unachotakiwa  kufanya ni kuamini tu.  Baada  ya kusoma kuhusu ‘manifestation’ nikaona ni jambo jema, nimeamua kuwashirikisha watu wazitumie nguvu zilizo ndani yao kufanya mambo makubwa na kujiletea maendeleo. 

Mada hii ya ‘manifestation’, itakupa fursa ya kutumia nguvu ya mawazo yako kufungua nguvu zilizomo ndani yako kukuletea mafanikio kwenye maisha yako. Kwa  urahisi kabisa, kitu pekee unachotakiwa kuwa nacho ni imani, kuamini kuwa unaweza. Umeumbwa  na nguvu na uwezo wa Kimungu uliomo ndani yako na unaweza kuufungulia na kuutumia kujipatia mafanikio na kujiletea maendeleo. 

Nguvu ya ‘manifestion’ ni kutumia tu mawazo, kutengeneza ndoto za mafanikio na kutumia nguvu iliyomo ndani yako kuifanya ndoto yako iwe kweli, hivyo kutimiza ndoto yako. 

Mfano, unataka kupata fedha nyingi, uwe Tajiri. Kupitia  ‘manifestation’, unawaza tu jinsi ya kupata pesa kisha unaamini utapata pesa. Unaweka  juhudi kwenye kutafuta pesa, kisha nguvu za Mungu zilizomo ndani yako zitakufungulia milango ya shughuli za kupata pesa, hatimaye utapata pesa na kuuaga umasikini. 

Upataji pesa kupitia ‘manifestation’, si kuamini tu na kulala kitandani kisha ukiamka asubuhi, unakuta umeletewa pesa chini ya mto! Katika kupata mafanikio kupitia ‘manifestation’, kuna misingi yake saba ambayo ni sheria, kanuni zake na utaratibu wake wa utekelezaji, hivyo lazima ufanye bidii kukipata kile unachotaka. 

Tukutane wiki ijayo, nitakapokuletea kwa undani misingi saba ya ‘manifestation’. Kitu  muhimu ni kukumbuka kuwa kila binadamu amekuja duniani akiwa mtu na ataondoka mtupu. Kupata  na kukosa, ni juhudi tu na maarifa kama haya.

Wasalaam

Paskali

075427040