Viko vitu vya kupenda lakini si mke wa mtu

By Adam Fungamwango , Nipashe Jumapili
Published at 04:45 PM Feb 04 2024
Cheating
Mtandao
Cheating

"KUMPENDA mke wa rafiki yako kweli ni hatari, viko vitu vya kupenda lakini vingine vina madhara, oooh moyo utakupeleka kaburini."

Hicho ni kiitikio cha wimbo uitwao, 'Ushinde moyo wako', uliopigwa na OTTU Jazz, wana wa Msondo Ngoma, utunzi wake marehemu, Tx Moshi William.

Wimbo huu ulirekodiwa mwanzoni mwa miaka ya 1990, lakini maana na maudhui yake yataishi milele, dahari hadi mwisho wa dunia hii.

Unawaasa watu wenye tabia ya kupenda au kutongoza wake za wake za watu. Wengine wanakwenda mbali zaidi wanawachukua mpaka wake za rafiki zao. 
 Kama Tx Moshi alivyobainisha hapo kuwa kitu hicho ni cha hatari kwa sababu inawezekana kabisa kinaweza kumpeleka mtu kaburini.

Ndiyo maana wapo waliobainisha kuwa mke wa mtu ni sumu. Maana yake mwenyewe akigundua anaweza kufanya chochote kinachoweza kuhatarisha maisha yake mwenyewe, mkewe au yule aliyefanya kitendo hicho.


Na kitu kama hicho hakiwezi kutafsiriwa vyovyote vile zaidi ya tamaa na ugomvi, kwani wanawake waliojaa katika dunia hii ya Mungu leo kwenda kuchukua mwanamke ambaye ameolewa tayari au mke wa mtu unayemfahamu?

Vitu kama hivi vimetokea sana kwenye jamii na tumeshuhudia kusababisha matatizo makubwa kwa wahusika na hata jamii kwa ujumla.

Kwanza kabisa, mwenyewe akijua anaweza kuchukua uamuzi ya kujimaliza mwenyewe. WaKo ambao hawana uvumilivu hata chembe, wao wanaamua kujidhuru.

Wengine hawana tabu, wao wanatoa talaka tu. Unaweza ukadhani labda hii ni afadhali kwa sababu kunakuwa hakuna maafa, lakini athari zake ni kwamba mume na mke wanaachana kwa sababu ya mpuuzi fulani, mwanamke anahangaika kwa sababu amedanganya na kutelekezwa, lakini pia kama wana watoto pia wanaanza kuteseka kwa kukosa malezi mema.

Mbaya zaidi kule wale wenye visasi. Asipomfanyizia mkewe, atafanya kila njia kumfanyizia yoyote aliyefanya kitendo hicho kwa mkewe.

Tumeshuhudia watu wakifanyiwa vitendo vibaya, wengine wakitekwa, wapo wanaouawa na hii yote ni kwa sababu ya visasi vinavyosababisha na mambo hayo.
 Waswahili wana msemo wao, 'cheza na mtu, usicheze na mke wa mtu.' Hawatanii, wanamaanisha kweli.

Hivi majuzi tu tumesikia mtu mmoja amehukumiwa kwa kuua watu saba wa familia moja. Kisa alikwenda kulipa kisasi cha kumuua mmoja wa watu wa familia hiyo kwa madai ya kuwa anatembea na mkewe.

Kilichotokea ni kwamba alikuwa anaua wengine kwa ajili ya kupoteza ushahidi, kwani baadhi walimuona na wengine walikuwa anapiga kelele. Ni jambo la kusikitisha sana.  Aliyeua hakufanya vyema na aliyeuawa naye 'alizingua', kutembea mke wa mwenzake. Matokeo yake wamesababisha vifo vya watu wasiohusika kabisa.

Si vizuri kama ukipatwa na jambo hilo kulipiza kisasi badala yake vipo vyombo vya sheria kwa ajili ya kufuata mkondo wake. Lakini wenye tabia hii wanatakiwa waache kwa sababu wanajiweka kwenye hatari zaidi kuliko furaha ya muda mfupi wanayoipata.

Ukisoma mashairi ya wimbo wa Msondo unaonya kila kitu, unaweza kupitia hapa.

"Usiendekeze ee moyo utakavyokutuma. Unadanganya jaribu kushinda, usiposhinda, huna budi kumia, utajivisha kitanzi pasipo huruma."

"Kumpenda mke wa rafiki yako kweli ni hatari, viko vitu vya kupenda lakini vingine vina madhara, oooh moyo utakupeleka kaburini. Nakuomba jirekebishe bwana, tabia hiyo siyo nzuri bwana, ni kitendo cha aibu na kashfa ya hali ya juu, tunakusihi sana acha mara moja.

Ulijua huyo ni ndugu yako na rafiki yako swahiba na leo wamasaliti, vipi sasa wanamtamani shemejiyo? Sikio la kufa halisikii dawa."

Hata mwanamuziki Marijani Rajab hakukaa kimya kwenye hili. Miaka ya 1980 alitunga wimbo aliouita 'Mwana Umepotea,' ambao una mashairi haya.

"Mzee Said ee alikuja lalamika ee, kasikia fununu kwamba unavuruga nyumba za watu kaja kutoa onyo anasema kijana ole wako, nasikitika sana ndugu yangu kuwa na mambo hayo, umefanya mambo mengi lakini haya yamezidi kipimo, mchezo na nyumba za watu sawa sawa kucheza na moto. Wacha wacha mara moja, hatari kubwa. Utapoteza maisha baba, na wewe ungali mdogo, hujaiona dunia baba, chonde chonde nakuomba baba."

Kaka anamwambia mdogo wake kuwa mjumbe mzee Said alikwenda nyumbani kwao kulalamika juu ya tabia ya kijana huyo kucheza na nyumba za watu. Maana yake anachukua wake za watu. Marijani akamuasa kuwa tabia hiyo ni sawa na kucheza na moto, matokeo yake atapoteza maisha wakati bado ni kijana mdogo.

Huyu ni kijana wa mwisho aliyedekezwa kiasi kwamba tabia yake ikawa mbaya, akawa anafanya kila kitu kibaya mama wizi na mambo mengine kama ulevi, huku akikingiwa kifua na mama yao.

Matokeo yake sasa akajiingiza kwenye janga la kutamani wake za watu.

"Ewe kipenzi cha mama ee, ewe ndugu yetu kitinda mimba, hebu tizama unavyofanya kwanza. Mbona nakuona unapotea, mama naye mapenzi kazidisha kwako, hata kukukanya anashindwa, anakuacha ufanye unavyotaka mwana.

Sasa imebidi nikueleze, nakwambia kama mimi ni kaka yako, ingawa natambua unanidharau, lakini mimi ndiyo nimeona dunia mwanzo." Hicho ki kipande cha kwanza wimbo huo. Narudia, mke wa mtu ni sumu.

Tuma meseji 0716 350534