Wafanyabiashara mtajificha kwenye hicho kichaka hadi lini?

By Godfrey Mushi , Nipashe Jumapili
Published at 05:00 PM Apr 14 2024
Fedha.
PICHA: MAKTABA
Fedha.

WATANZANIA walio wengi wamekuwa wakitumia muda wao mwingi kufikiria kuhusu fedha, hatua ambayo imewafanya muda wote kushikwa na wasiwasi inakuwaje wakikosa.

Jambo hilo linawaumiza kichwa kwa sababu hawana fedha ya kutosha, hasa wakati wanapokweenda dukani au sokoni na wanapokutana na bei za vitu wanavyovitaka viko juu.

Serikali nayo inatumia muda mwingi kufikiria kuhusu fedha hiyo hiyo kwa madhumuni tofauti na baadhi ya watu wanavyofikiria.

Rais Samia Suluhu Hassan naye amenukiliwa akisema: “Nilipomwapisha Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), nilimwambia nenda kakusanye kodi. Tunazihitaji  kwa ajili ya maendeleo lakini kodi za dhuluma hapana.

“Nilisema hivyo kwa kutambua serikali inahitaji mapato yatokanayo na kodi ili kutimiza majukumu yake, ikiwamo kuhakikisha wananchi wanapata huduma za kijamii.  “Nilisisitiza haki kwenye ukusanyaji wa kodi nikiamini kwenye dhuluma baraka za Mungu hazipo. Leo  miaka mitatu baadaye napenda kusisitiza msimamo wangu wa kutokukubaliana na kodi za dhuluma.

“Nafarijika tangu tulipoanza kusisitiza ukusanyaji wa kodi kwa haki, makusanyo yanaendelea kuongezeka; kwa mfano makusanyo yamepanda kutoka Sh. trilioni 18 mwaka 2021 hadi Sh. trilioni 24  mwaka 2022.” 

Jambo muhimu kwa jamii nyingi ni kuwa na maisha mazuri au kuongeza kipato kwa kadiri inavyowezekana.

Unaweza kujiuliza pato halisi ni kitu gani, jibu ni uwezo wa kujipatia bidhaa na huduma kwa mtu mmoja mmoja. Sasa nyie mnaokwepa kulipa kodi mtajificha hadi lini?

Bei za mahitaji kama chakula, nishati na malazi, ni miongoni mwa vinavyopanda kwa kasi kuliko vingine. Hivyo makundi ya watu wenye kipato cha chini hutumia kiasi kikubwa cha fedha wanachopata kwa ajili mahitaji hayo kuliko wale wenye kipato kikubwa.

Fedha ni njia tunayoitumia kununua mahitaji kwa matumizi yetu. Katika dunia ya sasa, uamuzi mbalimbali katika masuala ya kiuchumi, umekuwa ukifanyika kwa kutumia fedha.

Fedha hiyo imekuwa na nguvu katika manunuzi ya bidhaa na utoaji wa huduma hiyo ndio sababu noti na sarafu zimetambulika moja kwa moja kama fedha.

Kama tunatumia kiasi kikubwa cha fedha kununua mavazi, hii ina maana kuwa viwanda vya nguo vitakuwa kwa wingi.

Hata hivyo, kabla hatujatafakari suala la kodi, ni vyema tukafahamu kuhusu kupanda na kushuka kwa bei za bidhaa; hii inatokana na wengi wetu kupata wasiwasi pindi bei za bidhaa na huduma mbalimbali zinapoanda kila kukicha, huku kilio kikubwa kikiwaendea watu wenye vipato vya chini.

Kupanda kwa bidhaa na huduma husababisha kuporomoka kwa hali za maisha, ambapo itampasa mtu kununua bidhaa kidogo na kupata huduma kidogo kuliko ilivyokuwa kabla ya kupanda kwa bei.

Kwa mujibu wa Kanzidata ya Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS), mfumuko wa bei wa taifa kwa kipimo cha mwaka, unapima kiwango cha kasi ya mabadiliko ya bei za bidhaa na huduma zote zinazotumiwa na kaya binafsi.

Mfumuko wa bei wa taifa kwa mwaka ulioishia  Mei, 2023 umefika asilimia 4.0 kutoka asilimia 4.3 kwa mwaka ulioishia mwezi Aprili, 2023.

Hii inamaanisha kuwa kasi ya mabadiliko ya bei za bidhaa na huduma kwa mwaka ulioishia mwezi Mei, 2023 imepungua ikilinganishwa na kasi iliyokuwepo kwa mwaka ulioishia mwezi Aprili, 2023.

Fahirisi za bei zimeongezeka kutoka 108.42 mwezi Mei, 2022 hadi 112.72 mwezi Mei, 2023.  Kwa mfano, mwaka wa fedha 2022/2023, TRA ilivuka lengo la kukusanya hadi kufikia Sh. trilioni 24.76 kutoka Sh. trilioni 24.11 za mwaka wa fedha uliopita.

Makusanyo hayo ya nusu mwaka ni ongezeko la asilimia 11.5 ikilinganishwa na makusanyo ya Sh12.49 trilioni yaliyofikiwa katika kipindi kama hicho katika mwaka wa fedha uliopita, 2022/23. 

Ndiyo maana nasema tunapaswa kulitazama kundi hili lenye kipato cha chini ambalo mara kadhaa matumizi yao yamekuwa makubwa kuliko kile wanachokipata au tuseme hakilingani ili kukamilisha mahitaji yao kama chakula, malazi na mavazi.

        . Godfrey Mushi ni Mwandishi Mwandamizi wa Nipashe, Kanda ya Kaskazini. Anapatikana kwa simu namba 0715 545 490 au barua pepe: [email protected]