Benki ya Stanbic Tanzania yadhamini mbio za Run For Binti Race

By Mwandishi Wetu , Nipashe Jumapili
Published at 03:07 PM May 26 2024
Waziri wa Katiba na Sheria Balozi Dkt. Pindi Chana (kushoto) akimkabidhi zawadi mshindi wa kwanza wa mbio za Run for Binti Race kilomita 21 wanawake, Glory Sylvester kutoka Dar es salaam.
Picha: Mpigapicha Wetu
Waziri wa Katiba na Sheria Balozi Dkt. Pindi Chana (kushoto) akimkabidhi zawadi mshindi wa kwanza wa mbio za Run for Binti Race kilomita 21 wanawake, Glory Sylvester kutoka Dar es salaam.

Benki ya Stanbic Tanzania (SBT) ina furaha kutangaza udhamini wake wa mbio za "Run for Binti Race", ambazo huchangisha fedha kwa ajili ya wasichana wasiojiweza na kukuza uendelevu wa mazingira.

Mbio hizo zinalenga kushughulikia masuala ya maji na usafi wa mazingira mashuleni, kutoa taulo za kike kwa wanafunzi wa kike wasioweza kujigharamia kote nchini, na kupanda miti katika miji inayokabiliwa na matatizo makubwa ya mazingira.

Benki ya Stanbic, kama taasisi ya kifedha inayowajibika kijamii, imejitolea kuwa na matokeo chanya kwa jamii inayoihudumia. Lengo la benki ni kushughulikia changamoto muhimu za kijamii na kukuza maendeleo endelevu kwa kushirikiana na wadau na kutekeleza miradi ya kimkakati.

Mbio hizo zilifanyika jijini Dar es Salaam na kuwatanisha watu wa kada mbalimbali wakiwemo wanariadha, wakimbiaji wa kijamii, viongozi wa jumuiya na wafadhili wa makampuni kwa mbio za kilomita 5, 10 na 21. Mamia ya washiriki waliweza kuchangia tukio hilo kwa kujiandikisha kushiriki marathoni, ikiwa pamoja na ufadhili wa makampuni. 

“Tunafuraha kuunga mkono ‘Run for Binti Race’ na mipango yake ambayo inachangia kwa kiasi kikubwa ustawi wa wasichana wasiojiweza nchini Tanzania na wakati huo huo kuunga mkono mpango wa kijani wa upandaji miti katika miji yenye mahitaji makubwa.” Alisema Mkuu wa Kitengo cha Wateja Binafsi wa Benki ya Stanbic Tanzania, Omari Mtiga “Kupitia kazi yetu na Taasisi ya Legal Society Foundation (LSF), tunatarajia mpango huu utasaidia kwa kiasi kikubwa kuwawezesha wanawake na kupunguza matatizo ya mazingira katika miji yetu. Tunajivunia sana ushirikiano wetu na LSF kwani mbio hizi za marathoni ni mojawapo ya mipango yetu ya Uwajibikaji kwa Jamii (CSR) ambayo inaashiria dhamira ya SBT ya kuwekeza katika jamii zetu kama raia anayewajibika kwa jamii."

Benki ya Stanbic Tanzania (SBT) imetoa jumla ya shilingi milioni thelathini (TZS 30,000,000)kuelekea mbio hizo kama sehemu ya ufadhili na tutaendelea kufadhili miaka mitatu mingine ijayo.  Mapato ya mbio hizo, yatatumika kutoa Taulo za Kike kwa wanafunzi wasiojiweza katika miji iliyotambuliwa na mahitaji ya haraka; na kufadhili miradi ya upandaji miti katika miji yenye mahitaji ya dharura ya mazingira, kwa lengo la kupambana na ukataji miti, kukabiliana na mabadiliko ya hali ya hewa, na kuboresha afya kwa ujumla na uendelevu wa mifumo ikolojia ya ndani. Fedha hizo pia zitatumika kujenga vyoo vinavyohitajika sana katika shule maalum ili kuboresha usafi wa mazingira na usafi wa wanafunzi.

Stanbic Tanzania imechangia TZS 1 bilioni, katika kipindi cha miaka mitano iliyopita, ambazo zilitumika kujenga vyumba vya madarasa, kutoa madawati, kujenga vyoo shuleni na kusaidia wanawake nchini. 

Pia imetoa wito kwa wanajamii, washirika wa makampuni, na mashirika ya hisani kushiriki katika mbio za mwaka ujao za Run For Binti marathon na kuchangia. SBT inaamini kuwa kwa pamoja, sote tunaweza kuleta mabadiliko chanya na kujenga mustakabali bora wa kizazi chetu kijacho.

Kwa upande wake Waziri wa Katiba na Sheria, Mheshimiwa Balozi Dkt.Pindi Chana ambaye alikuwa mgeni rasmi kumuwakilisha Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe Dkt. Doto Biteko alisema “Napenda kutoa shukurani zangu za dhati kwa wadau wote wa mbio hizi  na kama ilivyoelezwa mbio hizi zimelenga kujenga  na kukuza  ustawi wa jamii  kielimu , kiafya na katika kutunza mazingira kupitia kuwezesha ujenzi wa vyoo bora na vya kisasa na ujenzi wa visima vya maji mashuleni, kutoa elimu ya utunzaji mazingira, kupanda miti na matumizi sahihi ya Nishati safi mashuleni , kutoa elimu ya kupinga masuala ya ukatili wa kijinsia pamoja na kutoa elimu ya hedhi salama na afya ya uzazi pamoja na watoto wakike kupata vifaa vya hedhi salama (reusable pads)  na kuwalinda na magonjwa lakini kuwawezesha kuhudhuria shuleni bila kukosa na kushindwa kufanya vizuri kwenye masomo yao”. 

Aliendelea kusema “Malengo haya yana tija muhimu katika kuendeleza ustawi wa jamii na ni dhahiri kwamba ukosefu wa taulo za kike kwa wasichana ni changamoto kubwa, Serikali inaendelea kukabiliana na kumaliza changamoto hii. Mashindano hayo yaliyoshindaniwa na washiriki kutoka maeneo mbalimbali ya nchi yaliweza kupata washindi kwa upande wa Kike 21Km aliongoza mshindi wa kwanza , Glory Sylvester(Dsm), wapili ni Arafa Msala(Dsm) na watatu ni Monica Lugendo (Dsm) na upande wa wanaume 21km yaliongozwa na Emmanuel Josephat, Mussa Ramadhani na Juma Cuthbert