Xavi kuwashtaki waandishi wa habari

By Mwandishi Wetu , Nipashe Jumapili
Published at 05:25 PM Mar 31 2024
KOCHA wa Barcelona, Xavi Hernandez.
PICHA: BNN
KOCHA wa Barcelona, Xavi Hernandez.

KOCHA wa Barcelona, Xavi Hernandez alithibitisha atachukua hatua za kisheria dhidi ya wanahabari wawili ambao alisema walitengeneza habari kumhusu yeye.

Taarifa ziliibuka wiki hii zikidai Xavi hakufurahishwa na ripoti moja iliyosema alidai aliwataka makocha wote wa timu yake kuweka simu zao mezani ili abaini nani anavujisha siri za klabu hiyo.

Habari nyingine ilihusu mwandishi wa habari ambaye alidai Xavi alimtumia ujumbe akilalamika kuhusu ukosoaji aliochapisha, ambao ulikanushwa na vyanzo vya karibu na bosi wa Barca.

"Ninaelewa ukosoaji lakini kuna mipaka," alisema Xavi katika mkutano na waandishi wa habari kabla ya mchezo wa LaLiga dhidi ya Las Palmas uliochezwa kwenye Uwanja wa Olimpiki jana.

"Sitavumilia uongo au watu kubuni vitu. Ni wakati wa kusema vya kutosha, ni uongo mkubwa, kwa hiyo sasa ni wakati wa kuchukua hatua."

Xavi amevikosoa vyombo vya habari mara kadhaa msimu huu, akipendekeza Disemba vyombo vya habari hasi vilikuwa vinaathiri uchezaji wa timu yake.

Baada ya kufika robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya mwezi huu, alitaja na kushutumu makala ya Desemba ambayo ilisema Barca ilikuwa na "mzaha" wa mashindano haya ya Ulaya.

Mazingira makali ya vyombo vya habari yanayoizunguka klabu hiyo yalikuwa moja ya sababu zilizochangia Januari kutangaza atajiuzulu mwishoni mwa msimu huu. 

Tangu wakati huo, Barca hawajafungwa katika mechi 10, na kutinga hatua ya nane bora ya Ligi ya Mabingwa Ulaya kwa mara ya kwanza tangu 2020 na kupanda hadi nafasi ya pili kwenye LaLiga, ingawa wamepitwa alama nane nyuma ya vinara Real Madrid.

Imesababisha wito kwa Xavi, ambaye aliiongoza Barca kutwaa ubingwa wa LaLiga msimu uliopita, kusitisha uamuzi wake na kujitolea kuinoa timu hiyo ya Katalunya mwakani.

"Ninashukuru watu wanataka nibaki, lakini hakuna kilichobadilika, ninafikiria maslahi ya klabu," aliongeza.

Kiwango cha hivi karibuni cha Barca kilichangiwa na kuibuka kwa Lamine Yamal na Pau Cubarsí, ambao wana umri wa miaka 16 na 17 na tayari ni wachezaji wa kimataifa na Hispania. 

Mshambuliaji Yamal alilipa taifa lake sare ya 3-3 Jumanne dhidi ya Brazil, akipokea pongezi kutoka Santiago Bernabéu.