Coastal Union yaongeza 'joto' kwa Simba, Yanga

By Adam Fungamwango , Nipashe Jumapili
Published at 03:05 PM Apr 14 2024
Mechi ya Mashujaa FC dhidi ya Coastal Union.
PICHA: MAKTABA
Mechi ya Mashujaa FC dhidi ya Coastal Union.

BAADA ya kupata ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Mashujaa FC, umeifanya Coastal Union kujiwekea katika mazingira mazuri ya kukata tiketi ya kushiriki mashindano ya kimataifa yanayoandaliwa na Shirikisho la Soka Afrika (CAF).

Ushindi huo wa Coastal Union pia unaweza kuzipa 'homa' vigogo vya soka nchini, Simba na Yanga pamoja na Azam FC zote za Dar es Salaam.

Mabao ya Shedrack Malungwe na Bakari Selemani yaliifanya Coastal Union ifikishe pointi 33, ikijikita katika nafasi ya nne ya msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara ikitangaza hali ya hatari kwa vinara Yanga, Simba na Azam, ambapo kama zitasuasua inaweza kutwaa moja kati ya nafasi tatu za juu walizozishikilia.

Mabingwa hao wa Tanzania Bara mwaka 1988, walikuwa vibonde katika mzunguko wa kwanza, walibadilika ghafla mzunguko wa pili ulipoanza kutokana na kufanya usajili mzuri kipindi cha dirisha dogo pamoja na kumwajiri Kocha Mkenya, David Ouma.

Mashujaa FC, ambayo iliiondoa Simba kwenye Kombe la FA, Jumanne iliyopita kwa mikwaju 6-5 ya penalti, baada ya sare ya bao 1-1, ilishindwa kabisa kukabiliana na vijana machachari wa Ouma.

Endapo itashinda mechi zake nane zilizosalia, Coastal Union itafikisha pointi 67, hivyo timu za Yanga, Simba na Azam kama zinataka kushikilia nafasi hizo tatu za juu, inabidi nazo zishinde mechi zao, ili kuepuka kuenguliwa.

Coastal Union imebakiza mechi za nyumbani dhidi ya Prisons (Mei 8, mwaka huu), Singida Fountain Gate (Mei 20), JKT Tanzania (Mei 27) na KMC (Mei 30), huku za ugenini zikiwa ni dhidi ya Namungo, (Aprili 17), Yanga (April 27), Geita Gold (Mei 15) na Kagera Sugar (Mei 21).

Ligi Kuu Tanzania Bara inatarajia kuendelea tena leo kwa mabingwa watetezi, Yanga kucheza dhidi ya Singida Fountain Gate wakati Namungo watawakaribisha Azam FC kwenye Uwanja wa Majaliwa ulioko Ruangwa mkoani, Lindi.