Mnunka: Nilifikiria kufunga mabao 25

By Saada Akida , Nipashe Jumapili
Published at 09:51 AM May 26 2024
Mshambuliaji wa timu hiyo, Aisha Mnunka.
Picha: Mtandao
Mshambuliaji wa timu hiyo, Aisha Mnunka.

WAKATI Simba Queens wanahitaji pointi moja ili kujihakikisha ubingwa wa Ligi Kuu ya Wanawake Tanzania msimu huu, kinara wa kupachika mabao, mshambuliaji wa timu hiyo, Aisha Mnunka, amesema malengo yake makuu ni kuona wanatwaa taji la msimu huu.

Mnuka na Stumai Abdallah wa JKT Queens, wote wakiwa Watanzania wanachuana vikali kuwania kiatu cha dhahabu.

Straika huyo wa Simba Queens akiwa ametikisa nyavu mara 18 wakati Stumai amefunga magoli 16.

"Nikipata nafasi natumia kwa sababu nataka timu yangu ishinde, lakini lengo langu la pili ni kuwa mfungaji bora, mwanzoni malengo yangu yalikuwa kufunga mabao 25, naona natakiwa kuzidisha ili kuwa mfungaji bora," alisema Mnunka.

Katika msimamo wa ligi hiyo itakayorejea tena dimbani kuanzia Juni 7, mwaka, Simba Queens inaongoza ikiwa na pointi 43 na JKT Queens, mabingwa watetezi wakiwa nafasi ya pili na pointi 34 kibindoni.