Nyota Simba wanukia Singida

By Adam Fungamwango , Nipashe Jumapili
Published at 09:36 AM Jun 09 2024
Kocha mpya, Patrick Aussems,
Picha: Mtandao
Kocha mpya, Patrick Aussems,

BAADA ya kutangazwa rasmi kutua katika kikosi cha Singida Black Stars, Kocha mpya, Patrick Aussems, raia wa Ubelgiji amesema anatarajia kusajili baadhi ya wachezaji ambao aliwahi kufanya nao kazi katika kikosi cha Simba.

Aussems ametumia Singida Black Stars akichukua nafasi ya Mecky Maxime.

Ofisa Mtendaji Mkuu wa Singida Black Stars, Kassano Jonathan, amesema kocha huyo anaendesha zoezi la usajili akishirikiana na menejimenti ili kupata wachezaji ambao watakifanya kikosi chao kuwa imara na tishio katika msimu ujao.

"Kwa sasa Kocha Aussems ndiye anayeongoza zoezi la usajili kwa kushirikiana na menejimenti, baada ya kumtangaza kuwa kocha mkuu. Tumeingia naye makubaliano ya mwaka mmoja ambao utaanza Julai Mosi, mwaka huu, na utamalizika Juni 30, mwakani," alisema Kassano.

Ofisa huyo alisema tayari Aussems ameshaanza mchakato wa usajili kwa kutuma mapendekezo ya wachezaji anaowataka wawe wamesajiliwa kabla ya yeye kuwasili nchini kuanza kazi.

Aussems amerejea nchini akitokea AFC Leopards inayoshiriki Ligi Kuu ya Kenya, ambayo imemaliza msimu huu ikiwa nafasi ya saba na pointi 36.