Simba Queens yachekelea ubingwa, yawaita Chamazi

By Somoe Ng'itu , Nipashe Jumapili
Published at 09:31 AM Jun 09 2024
news
Picha: Simba SC
Wachezaji wa Simba Queens wakifurahia baada ya kuifunga Alliance Girls mabao 3-0 katika mechi iliyochezwa kwenye Uwanja wa CCM Kirumba jijini, Mwanza juzi na kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu ya Wanawake Tanzania msimu huu.

WACHEZAJI wa Simba Queens wamesema wanasikia furaha kutimiza malengo yao ya kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu ya Wanawake Tanzania msimu huu na wanawaomba mashabiki na wanachama wao kujitokeza kusheherekea kombe hilo kesho kwenye Uwanja wa Azam Complex, Dar es Salaam.

Simba Queens imeivua ubingwa JKT Queens baada ya kuifunga Alliance Girls mabao 3-0 katika mechi ya ligi hiyo iliyochezwa kwenye Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza juzi na kufikisha pointi 46, ambazo hazitafikiwa na timu nyingine msimu huu.

JKT Queens ambayo jana iliwafunga Fountain Gate Princess mabao 4-0 yenye ina pointi37, kila timu ikibakiwa na michezo miwili ili kumaliza msimu wa 2023/2024.

Akizungumza baada ya mechi juzi, straika wa Simba Queens, Aisha Mnunka, alisema wanafuraha kufikia malengo yao na kama wasingetwaa ubingwa huo, wangeumia sana.

Mnunka amewaomba mashabiki wa Simba kujitokeza kwa wingi kesho katika mechi yao dhidi ya Fountain Gate Princess ili kuendeleza shangwe.

Alisema wametwaa ubingwa kwa sababu waliweka malengo hayo tangu kuanza kwa msimu huu.

"Tunafuraha sana kutwaa ubingwa, tumejisikia raha sana kufikia malengo, kama tusingeshinda leo (juzi), au tungeshindwa kutwaa ubingwa tungeumia sana kama tulivyoumia katika msimu uliopita, naombeni mashabiki mje kwa wingi Chamazi kama mlivyojitokeza hapa (Mwanza)," alisema straika huyo.

Naye golikipa wa Simba Queens, Caroline Rufo, alisema anafuraha kuisaidia timu yake kutwaa ubingwa wa ligi hiyo ambayo ilikuwa na ushindani.

"Nafurahia kutoruhusu bao katika mechi ya leo (juzi), na mechi nyingine kwa sababu zimesaidia timu yangu kupata ubingwa, tunawashukuru sana mashabiki wote kwa kutuunga mkono," alisema Rufo.

Kwa kutwaa ubingwa huo, Simba Queens itaiwakilisha Tanzania Bara katika mashindano ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati (CECAFA) ili kupata timu itakayochuana katika Fainali za Ligi ya Mabingwa Afrika kwa Wanawake.