Simba yauweka ubingwa rehani

By Adam Fungamwango , Nipashe Jumapili
Published at 02:11 PM Apr 14 2024
Mshambuliaji wa Simba, Fred Michael (jezi nyekundu), akiwania mpira dhidi ya beki wa kati wa Ihefu, Benjamin Tanimu katika mechi ya Ligi Kuu Tanzania Bara iliyochezwa kwenye Uwanja wa CCM Liti mkoani, Singida jana. Timu hizo zilitoka sare ya bao 1-1.
PICHA: SIMBA SC
Mshambuliaji wa Simba, Fred Michael (jezi nyekundu), akiwania mpira dhidi ya beki wa kati wa Ihefu, Benjamin Tanimu katika mechi ya Ligi Kuu Tanzania Bara iliyochezwa kwenye Uwanja wa CCM Liti mkoani, Singida jana. Timu hizo zilitoka sare ya bao 1-1.

MASHABIKI wa Wekundu wa Msimbazi walilazimika kusubiri dakika nane kabla ya mechi kumalizika ili kushuhudia timu yao ikipata bao la kusawazisha dhidi ya Ihefu SC katika mechi ya Ligi Kuu Tanzania Bara iliyochezwa kwenye Uwanja wa CCM Liti mkoani, Singida jana.

Alikuwa ni Clatous Chama aliyefunga kwa penalti dakika ya 82 na kuifanya mechi hiyo kumalizika kwa sare ya bao 1-1, huku yeye mwenyewe akifikisha magoli saba mpaka sasa kwenye orodha ya wafungaji wa ligi hiyo msimu huu.

Kabla ya hapo, mashabiki wa timu hiyo walikuwa wamekaa 'roho juu' tangu dakika ya 41 ambapo wenyeji Ihefu walipopata bao la kuongoza.

Zilikuwa ni juhudi binafsi za Kibu Denis, aliyekuwa nyota wa mchezo wa jana kwa upande wa Simba, aliyeangushwa ndani ya eneo la hatari na beki wa kati wa Ihefu, Mukrim Issa, na mwamuzi kuamuru adhabu hiyo ambayo ilibadilisha ubao wa matokeo.

Bao hilo liliinusuru Simba kupata kipigo cha nne mfululizo, kwa sababu ilifungwa mara mbili na Al Ahly ya Misri, nyumbani bao 1-0 na ugenini mabao 2-0 katika mechi ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika, kabla ya kuondoshwa tena katika michuano ya Kombe la FA kwa kuchapwa penalti 6-5 dhidi ya Mashujaa FC, Jumanne iliyopita.

Matokeo ya jana yanaifanya Simba kuongeza pointi moja na kufikisha 46, ikibaki pale pale katika nafasi ya tatu ya msimamo wa ligi, ikifikisha mechi 20.

Sare hiyo, imeipandisha Ihefu kutoka nafasi ya 11 hadi ya tisa ikiwa na pointi 24 kibindoni.

Mchezo ulianza kwa Ihefu kuonekana hawana wasiwasi, badala yake walikuwa wakigongeana pasi fupi fupi na ndefu kiasi cha dakika moja kupita bila wachezaji wa Simba kuugusa mpira.

Dakika ya nne Simba ilifika langoni kwa Ihefu kwa mara ya kwanza na kukosa bao la wazi kupitia straika wake, Fredy Michael, aliyeupata mpira nje ya eneo la hatari akiwa peke yake, akaingia nao ndani, lakini alitumia muda mrefu kufikiria kupiga hadi alipofika hatua nne toka kwa kipa, Aboubakar Khomeny, kabla ya beki Benson Mangolo, kuufagia.

Dakika moja baadaye Ihefu ilijibu shambulizi hilo kupitia kwa straika wake, Elvis Rupia, aliyewachachafya mno mabeki wa Simba jana, baada ya kuunganisha moja kwa moja krosi ya Morice Chukwu, lakini mpira ukapaa juu ya lango.

Simba iliendelea kukosa mabao ya wazi, dakika ya tano kupitia kwa Freddy tena, na dakika ya 20, alipomiminiwa krosi na Chama, lakini baada ya kuuweka mpira wavuni, akamchezea madhambi, Khomeny.

Sadio Kanoute naye pia alikosa bao dakika ya 21, baada ya kazi nzuri iliyofanywa na Saido Ntibazonkiza ya kumwekea pasi ya nyuma, ambapo alipiga shuti kubwa lililopita juu ya lango la Ihefu.

Shuti la kwanza la Ihefu lililolenga lango ndiyo lililozaa bao dakika ya 41, lililowekwa wavuni na Duke Abuya aliyeitendea haki krosi ya Mkenya mwenzake, Rupia.

Lilikuwa ni kosa la kipa wa Simba, Ally Salim kuufuata mpira huo wa krosi, lakini akaukosa, ukamkuta Duke ambaye alimwacha akiwa ameanguka chini, akamlamba chenga beki, Fondoh Cha Malone na kuujaza wavuni kirahisi.

Kipindi cha pili kila timu ilifanya mabadiliko kadhaa ambayo yaliongeza spidi ya mpira, Luis Miquissone wa Simba kama angekuwa na bahati angeipatia timu yake mabao mawili, dakika ya 78, alipiga shuti kali akiwa ndani ya eneo la hatari ambalo Khomeny alilipangua na dakika mbili kabla ya mechi kumalizika, shuti lake lilioonekana kwenda wavuni, liliwababatiza mabeki wa Ihefu na kupaa juu kidogo ya lango.

Baada ya mechi hii, Simba inakwenda kujiandaa kuwakabili watani zao wa jadi, Yanga, mechi itakayochezwa Aprili 20, mwaka huu kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam.