Yanga kupiga kambi Ulaya, kufanya ziara Kenya, Sauzi

By Adam Fungamwango , Nipashe Jumapili
Published at 08:54 AM Jun 16 2024
Ofisa Habari na Mawasiliano wa Klabu hiyo, Ali Kamwe.
Picha: Maktaba
Ofisa Habari na Mawasiliano wa Klabu hiyo, Ali Kamwe.

KIKOSI cha Yanga kinatarajiwa kufanya ziara nchini Kenya na Afrika Kusini, huku safari hii kikiweka kambi yake barani Ulaya, tayari kwa msimu mpya wa mashindano msimu ujao.

Akizungumza jana jijini Dar es Salaam, Ofisa Habari na Mawasiliano wa Klabu hiyo, Ali Kamwe, amesema safari hii kambi yao haitokuwa Kigamboni kama ilivyo kawaida, badala yake wataelekea barani Ulaya, tayari kwa maandalizi.

"Napenda niwafahamishe wanachama na mashabiki wa Yanga kuwa tunatarajia kufanya ziara nchini Afrika Kusini kwa mwaliko wa klabu ya Mamelodi Sundowns,  tuna mialiko pia nchini Kenya kwenye ufunguzi wa uwanja, na safari hii tutakwenda kuweka kambi yetu Ulaya, ni nchi gani? tutakuja kuwajulisha, ila kambi yetu msimu wa maandalizi haitakuwa Kigamboni, badala yake wachezaji watakutana Kigamboni baada ya mapumziko yao na baadae kuanza safari ya kwenda Ulaya," alisema Kamwe.

Akizungumzia usajili alisema watafanya usajili makini na kwa bahati nzuri, dirisha la usajili limefunguliwa kipindi cha kuanza mwaka wa fedha kwa klabu hiyo.

"Usajili umefunguliwa na mwaka wetu wa fedha wa klabu unaanza Julai Mosi, uliomalizika hatukuwa na majina makubwa, ila tulikuwa na wachezaji bora kama Pacome Zouzoua, Maxi Nzengeli na Yao Koassi, uwezo wao uliwashtua Watanzania. sisi hatuendeshwi na propaganda au mitandao ya kijamii, nimeuchungulia usajili wetu kidogo nimeona majina ya wachezaji wasio na majina makubwa lakini ni bora, pia wenye majina makubwa msimu ujao wapo tutakuwa nao," alisema Ofisa Habari huyo.

Yanga pamoja na kutwaa Ubingwa wa Tanzania Bara mara ya tatu msimu huu, lakini imekuwa na kiwango bora na msimu wenye mafanikio, ambapo mbali na ubingwa huo, imetwaa Kombe la FA, pamoja na kufika robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika, ikitolewa kwa mbinde na Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini.

Kwa mujibu wa viongozi wa klabu hiyo, wanataka kutengeneza kikosi bora zaidi kuliko msimu uliopita ili kuvuka mafanikio waliyoyapata msimu uliopita.