Yanga, Singida FG hesabu uwanjani

By Saada Akida , Nipashe Jumapili
Published at 02:40 PM Apr 14 2024
Yanga, Singida FG hesabu uwanjani leo.
PICHA: MAKTABA
Yanga, Singida FG hesabu uwanjani leo.

MABINGWA watetezi wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Yanga wanahitaji kuvuna pointi tatu muhimu katika mchezo wa ligi hiyo dhidi ya wenyeji Singida Fountain Gate FC utakaochezwa leo kwenye Uwanja wa CCM Kirumba jijini, Mwanza.

Yanga inahitaji ushindi ili kuendelea kujiimarisha kileleni katika vita ya kuwania taji la Ligi Kuu wakati wapinzani wao wanataka kuvuna pointi tatu ili kujiweka katika mazingira mazuri kwenye msimamo wa ligi hiyo.

Akizungumza na Nipashe, Kocha Mkuu wa Yanga, Miguel Gamondi, amesema amekiandaa vyema kikosi chake na wachezaji wote wapo tayari kwa ajili ya kusaka pointi tatu muhimu na si jambo lingine.

Gamondi amesema licha ya kukosa maandalizi mazuri kuelekea mchezo wa leo kwa sababu ya kutumia muda mrefu safarini baada ya kumaliza mchezo uliopita, bado anaamini nyota wake watapambana ili kupata ushindi.

“Nawaheshimu Singida Fountain Gate, tumefanya maandalizi mazuri na ya msingi, muhimu ni kushinda mechi ya kesho (leo) ili kuendelea kusalia katika uongozi wetu wa ligi hiyo,” amesema Gamondi.

Naye Kocha Msaidizi wa Singida Fountain Gate FC, Ngawina Ngawina, amesema wanacheza na timu kubwa na kwa kuzingatia hilo wamefanya maandalizi bora kuhakikisha wanaibana Yanga ndani ya dakika 90.

Ngawina amesema wachezaji wake wana hali nzuri wamejipanga kuhakikisha wanaishangaza Yanga katika mchezo huo.

" Tunahitaji pointi tatu, tunafahamu ubora wa Yanga, tutacheza kwa tahadhari kubwa ili kufikia malengo yetu katika mchezo huu. Kwa misimu hii miwili Yanga iko vizuri kila mmoja analifahamu hilo, hatuwaogopi, tunawaheshimuna,” amesema Ngawina.

Nyota wa Singida Fountain Gate, Habib Kyombo, amesema benchi la ufundi limemaliza jukumu lao na kazi iliyobaki ni kwao wachezaji kwenda kuonyesha mchezo mzuri ili kupata matokeo chanya. 

"Tuko tayari kupambana, safu yetu ya ushambuliaji iko vizuri, mchezo wa kesho (leo), utakuwa mzuri kwa sababu mwalimu ameandaa timu na mbinu, tunajua nini tunaenda kufanya katika mchezo huo dhidi ya Yanga,” amesema Kyombo.