Bashe atoa ufafanuzi mchele uliotoka Marekani

By Halfani Chusi , Nipashe
Published at 10:18 AM Mar 18 2024
Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe.
PICHA :Kilimo News
Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe.

SERIKALI imekanusha uvumi uliosambaa kwenye mitandao ya kijamii kwamba imekubali kupokea msaada wa chakula kutoka Serikali ya Marekani ikisisitiza nchi ina chakula cha kutosha.

Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe, ametoa kauli hiyo alipokuwa akielezea mafanikio ya miaka mitatu ya Rais Samia Suluhu Hassan katika sekta ya kilimo.

Amesema ameona kwenye mitandao ya kijamii mjadala mkubwa umeibuka kuhusu Tanzania kupewa msaada wa mchele na maharage uliowekwa virutubisho.

Akifafanua alisema chakula hicho ni mradi unaofanywa na shirika lisilo la kiserikali (NGO) na inafanya shughuli za miradi katika shule za msingi na sekondari.

“Sasa sisi tuliiambia ile NGO kwamba, nchi hii mchele upo na maharage yapo, zile pesa wanazozitumia kuwapa wakulima wa Marekani, wawape wakulima wa Tanzania. Tununue huo mchele na maharage kutoka hapa Tanzania halafu hivyo virutubisho wanavyotaka kuweka, tuweke hapahapa Tanzania wakati soțe tunaona,” amesema Bashe.

Akizungumzia uvumi unaoenezwa na baadhi ya wanasiasa kuwa serikali imewatekeleza vijana wa mradi wa Jenga Kesho Iliyobora (BBT), amesema imeibuka mijadala mingi na aliwaambia viongozi wake akiwamo Katibu Mkuu kwamba wasiogope hiyo ni sehemu ya kuboresha utendaji kazi wao.

Amesema kutoka na ukosefu wa ajira nchini, serikali ilikuja na mpango huo na haikutaka kulaumiwa na vijana kwamba waliomaliza chuo hawana ajira na kuondoa maswali yao ya wapi watapata kazi.

Bashe amesema kikwazo kikubwa kwa vijana baada ya kuanza kwa mradi huo kilikuwa ni ukosefu wa ardhi na kwamba kupitia hilo Rais wakati anazindua mradi huo, ardhi iliyokuwapo ilikuwa ni hekari 300 pekee, serikali ikafanya jitihada za kununua hekari zingine laki mbili ambazo mpaka leo zinatumika.

Amesema mpaka sasa vijana 260 wamewapeleka katika Shamba la Chinangali wamejengewa nyumba za kuishi kwa kuwa wamekubali kufanya shughuli za kilimo, na kila mwezi kijana anapewa Sh. 390,000 bure na serikali.

“Nimewaambia wanasiasa msiwatishe watoto wa masikini, kwa sababu wao wanakalia viti vyekundu akitoka tu anapata fedha wale ni watoto wa masikini wanahitaji kuwa na ‘future’. Nimewaambia vijana kule kama kuna mtu anataka kuingia kwenye siasa atoke aachane na masuala ya kilimo awaache ambao wapo committed kwenye kilimo,” amesisitiza.

Amesema serikali inaendelea kuandaa shamba la hekari 1,700 Chinangali na wamewajengea kiwanda, na Benki ya NMB imetoa Sh. bilioni 12 zitakazotumika kwa ajili ya ukarabati wa miundombinu na ununuzi wa mbolea.  

ALAMA ZA SAMIA

Amesema serikali imefanya mradi huo ni mikopo kwa vijana na kwamba kutokana na ugumu kwa mkulima mmoja mmoja kupata mitaji, Rais Samia aliamua kutoa fedha kupitia mfuko wa pembejeo na kuwakopesha kwa riba ya asilimia 4.5 mpaka sasa vijana 118 wamenufaika na serikali imewakopesha jumla ya Sh. milioni 970.

Amesema eneo la tatu la BBT ni ‘BBT Extension’. Serikali imeingia makubaliano na Chuo Kikuu cha kilimo sokoine (SUA). Vijana wanaomaliza wanawaingiza kwenye kampuni zinazonunua pamba, wanawaajiri na kuwalipa Sh. 500,000 kila mwezi. Mpaka sasa vijana 250 wameanza.

BAJETI YA KILIMO KUPAA

Bashe amesema Wakati Rais anaingia madarakani, eneo la umwagiliaji katika nchi lilikuwa hekta 726,000. Mwaka wa kwanza Rais alitoa fedha bajeti ya umwagiliaji zisizozidi Sh. bilioni 50 mpaka Sh. bilioni 361.

Kikubwa alichokifanya ni kuwekeza kwa kiwango kikubwa cha fedha ya umma kwenye kuendesha shughuli za uzalishaji.

Ameongeza bajeti kutoka Sh. Bil 290 hadi kufikia Sh. Bil. 750, na kwamba kwa mwaka huu bajeti ikafika hadi Sh. Bil. 970 na matarajio yao kwa mwaka ujao bajeti ya sekta ya kilimo ifikie Sh. Trilioni 1.

“Leo anafanya upembuzi yakinifu wa mabonde yote tuliyonayo ya nchi hii. Inawezekana asiyakamilishe yeye, atakuja kuyakamilisha mtu. Na hiyo ndio vision ya muda mrefu. Rais ameamua kuchukua ‘approach’ sahihi kwenye kilimo.

Amesema nchi itaandika historia kwa mara ya kwanza kufanya mradi wa kwanza wa kutumia maji kutoka Ziwa Victoria baada ya kukamilisha upembuzi yakinifu.

“Tunahahangaika ukame, kila siku mvua zikinyesha kuanzia Morogoro Dodoma hatupiti kuna maeneo tunaita yana ukame. Kwa mara ya kwanza mwaka huu serikali ya Awamu ya Sita imeanza ujenzi wa mabwawa 100 kuvuna maji ya mvua yanayomwagika barabarani.

“Pia tuna mradi wa kukusanya maji yanayojaa barabarani kwa ajili ya kupambana na ukame na kukuza kilimo cha umwagiliaji miradi hii imeshatangazwa na makandarasi wapo site.

Amesema lengo la serikali ndani ya miaka saba ijayo ni kuchimba visima 67,000 kwa ajili ya wakulima wadogo ambapo visima hivyo jumla vitatupatia ekari milioni 2.5 ambazo zitakuwa zinamwagiliwa lengo ikiwa ni kumfanya mkulima abaki shambani.

Kadhalika, ndani ya miaka mitatu ya serikali imefufua kampuni iliyoanzishwa na Baba wa Taifa ya Tanzania Fertilizer Company kwa kuipatia mtaji mwaka wa kwanza wastani wa Shilingi bilioni sita, mwaka wa pili ikapatiwa Sh. bilioni 40 na sasa mtaji umefika Sh. bilioni 116. Kampuni hiyo sasa, imekuwa moja ya kumi bora katika usambazaji wa mbolea nchini.

“Mwaka jana tumepata shida ya bei korosho kwenye Soko la Dunia na tumeauza kwa bei ya chini. Njia pekee hapa ya kumsaidia mkulima ni kuongeza thamani ya zao hili.

“Kwenye hili serikali imeanzisha mradi unaitwa ‘MARANJE’ na mpaka sasa tunatumia wastani wa Sh. bilioni 10 kwa ajili ya kujenga Maranje maghala yatakayosubiri mwekezaji alete mashine kwa ajili ya kubangua Korosho na malengo yetu ifikapo 2026/27 Korosho yote ibanguliwe nchini,” amesema.