DP World yaanza kazi bandari ya Dar

By Joseph Mwendapole , Nipashe
Published at 09:40 AM Apr 12 2024
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA), Plasduce Mbossa.
Picha: Maktaba
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA), Plasduce Mbossa.

KAMPUNI ya DP World ya Dubai imeanza rasmi kazi ya kushusha na kupakia makontena kwenye bandari ya Dar es Salaam.

Taarifa iliyotolewa jana na Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA), Plasduce Mbossa, ilibainisha hayo huku ikielekeza wateja wa bandari hiyo kuhusu masuala mbalimbali yakiwemo namna ya kufanya malipo kwa kampuni hiyo.

Taarifa hiyo inawaelekeza wateja na watumiaji wengine wa bandari kuhusu benki zitakazotumiwa na DP World kwa ajili ya malipo mbalimbali ya mizigo yao.

Kadhalika, taarifa hiyo imeonyesha wateja kuhusu mawasiliano mbalimbali yanayotumiwa na kampuni hiyo pamoja na ofisi zitakazotumiwa na maofisa wake.

Hivi karibuni, wafanyakazi wa TPA walipewa barua kuchagua kufanya kazi na mamlaka hiyo au kuhamia DP World itakapoanza kazi.

TPA iliwataka kuchagua ama kubaki katika ajira TPA au kusitisha mikataba na kujiunga na ajira mpya katika kampuni ya DP World.

Taarifa ya TPA iliyotolewa Machi 20, mwaka huu na Mbossa, ilisema Oktoba 22, 2023 mamlaka hiyo iliingia mkataba na DP World ya Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) kuhusu uendeshaji wa gati namba sifuri hadi tatu na gati namba nne hadi saba za bandari ya Dar es Salaam kwa kipindi cha miaka 30.

 “Kutokana na makubaliano hayo yanayohusisha usimamizi na uendeshaji wa maeneo tajwa, watumishi wa bandari ya Dar es Salaam,  wanapaswa kuchagua kati ya kubaki TPA au kusitisha mkataba wa ajira kati yao na  TPA au kusitisha mkataba wa ajira wa TPA na papo hapo kuajiriwa upya na DP World,” ilisema taarifa hiyo.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, uongozi wa TPA ulikuwa umekamilisha mchakato wa utoaji wa elimu kwa watumishi wote walio kwenye maeneo husika.

Taarifa pia ilisema mchakato wa utoaji elimu ulianza Machi 4 hadi 19, mwaka huu, kwa lengo la kuwapa watumishi wote uelewa sahihi wa mabadiliko ya uendeshaji yanayoendelea katika bandari ya Dar es Salaam.

“Pamoja na masuala mengine, elimu hii inahusisha mabadiliko ya uendeshaji wa bandari, utaratibu wa makabidhiano, utaratibu wa mtumishi kusitisha mkataba na TPA na papo hapo kuajiriwa upya na kampuni ya DP World kwa  mtumishi atakayekuwa ameamua kufanya hivyo kwa hiari yake mwenyewe bila kushurutishwa.

“Pia kuna stahiki ambazo zitatolewa na TPA kwa mtumishi atakayeamua kusitisha mkataba wa ajira wa TPA na kuajiriwa upya na Kampuni ya DP World.

“Watumishi watakaoamua kuajiriwa upya na kampuni ya DP World wanatakiwa kufika na kuorodhesha taarifa zao jengo la TPA Makao Makuu ukumbi wa mikutano ghorofa ya 32 kabla au ifikapo Machi 29, mwaka huu,” ilisema taarifa.