Bashungwa aagiza mabadiliko sheria

By Renatha Msungu , Nipashe
Published at 07:48 AM May 25 2024
Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa.
Picha: Mpigapicha Wetu
Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa.

WAZIRI wa Ujenzi, Innocent Bashungwa, ameishauri Bodi ya Usajili wa Wahandisi (ERB) kuirejesha bungeni sheria inayowasimamia kama wanaona ina upungufu ili ifanyiwe marekebisho yatakayoiwezesha kuwa na meno kwa wale wote wanaokiuka taratibu.

Bashungwa alitoa agizo hilo juzi jijini hapa, alipokuwa akifungua mkutano wa mwaka wa mafundi sanifu. 

Alisema  endapo bodi hiyo inaona sheria waliyo nayo ina upungufu, ni vyema kuipeleka bungeni ili kufanyiwa marekebisho. 

Alisema lengo la kusema hivyo ni kutaka kuwaweka sawa wahandisi ili waweze kufanya kazi zao kwa ufasaha na ufanisi pale wanapopata zabuni mbalimbali. 

"Angalieni sheria yenu vizuri kama mnaona ina upungufu basi iwasilisheni bungeni ifanyiwe marekebisho yatakayosaidia kuwa na makali ya kuwawajibisha wanaokiuka taratibu," alisema Bashungwa. 

Aidha, alisema wahandisi wote wanatakiwa kujisajili ili waweze kutambulika ikiwemo kujiunga na wenzao kwa ajili ya kufanya kazi mbalimbali za miradi. 

Kadhalika, alisisitiza suala la wahandisi kujisajili katika Bodi yao na kuongeza kuwa waliosajiliwa watumie kiapo vizuri katika ufanyaji kazi zao. 

Katika hatua nyingine Bashungwa alisema wahandisi 2,785 waliosajiliwa idadi hiyo ni ndogo, hivyo wanapaswa kuhimiza watu wajisajili ili watambulike. 

Waziri Bashungwa pia aliisisitiza bodi hiyo kuwawajibisha wahandisi wanaokwenda kinyume na taratibu na sheria za kazi na kuongeza kuwa wasipofanya hivyo watakuwa wanalea wahandisi waharibifu. 

Msajili wa ERB,  Bernard Kavishe, alisema bodi hiyo itaendelea kuwawajibisha wahandisi wanaokwe da kinyume na taratibu za kazi kama ilivyo ada. 

Alisema mkutano huo wa sita wanakwenda kujadili mambo muhimu ambayo yanakwenda kuimarisha utendaji wa kazi zao za kila siku. Pia aliwataka wahandisi kila mmoja kusikiliza kwa makini,ikiwemo kutoa maoni yao pale wanapohitajika kufanya hivyo. 

"Naomba msikilize kwa makini kile mnachofundishwa kwenye mkutano wenu na mtoe maoni," alisema Mhandisi Kavishe.