Benki ya Mwanga Hakika yazindua mikopo kwa wajasiriamali nchini

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 09:47 AM May 28 2024
Mkuu wa Idara ya Mikopo, Yonah Mgongolwa (kushoto), Mkuu wa Idara ya Wateja Wadogo na wa Kati wa Benki ya Mwanga Hakika, Mwinyimkuu Ngalima (katikati) na Mkuu wa Idara Biashara, Projest Massawe, wakizindua huduma rahisi ya mikopo kwa wajasiriamali wadogo.
Picha: Mpigapicha Wetu
Mkuu wa Idara ya Mikopo, Yonah Mgongolwa (kushoto), Mkuu wa Idara ya Wateja Wadogo na wa Kati wa Benki ya Mwanga Hakika, Mwinyimkuu Ngalima (katikati) na Mkuu wa Idara Biashara, Projest Massawe, wakizindua huduma rahisi ya mikopo kwa wajasiriamali wadogo.

KATIKA kuwezesha biashara nchini, Benki ya Mwanga Hakika imeleta sokoni huduma ya mikopo rahisi kwa wajasiriamali wadogo na wa kati ili kuwakwamua kiuchumi ijulikanayo kama Fursa Loan.

Huduma hiyo inakuja wakati ambao Watanzania wengi wamekuwa wanahitaji huduma za mikopo yenye riba nafuu na dhamana zinazoendana na aina ya biashara zao.

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa huduma hiyo wiki iliyopita, Mkuu wa Wateja Wadogo na wa Kati wa Mwanga Hakika Bank, Mwinyimkuu Ngalima, alisema benki hiyo imejizatiti katika kuleta huduma zinazokidhi mahitaji ya makundi mbalimbali ya wateja.

"Tunafarijika kuja na huduma hii ya mkopo kwa wajasiriamali wadogo na wa kati ambayo ni mikopo yenye gharama nafuu na dhamana zake zinalingana na aina ya biashara zao. 

"Tunaamini huduma hii inakwenda kuwa msaada mkubwa kwa wajasiriamali wadogo na wa kati kama mamalishe, bodaboda, madereva wa magari madogo ya biashara na wengineo ambao wamekuwa wanashindwa kupata mikopo kutokana na gharama kubwa na  kutokuwa na dhamana," alisema.

Ili mteja aweze kupata mkopo kwenye benki, anahitaji kuwa na dhamana ya mali isiyohamishika kama vile nyumba zenye hati miliki au mashine (kiwanda) jambo ambalo limekuwa likiwakosesha mikopo wafanyabiashara wadogo wasio na dhamana hizo.

Alsiema huduma hiyo inatoa fursa ya kipekee kwa wafanyabiashara wadogo na wa kati kupata mikopo yenye gharama nafuu na dhamana rahisi itakayowawezesha kuongeza mitaji kwenye biashara zao ili zikue zaidi. 

"Tunawakaribisha wajasiriamali wote bila kujali aina ya biashara kutumia fursa hii ili wakukuze biashara zao kwa kuongeza mitaji," alisema.

Tanzania inakadiriwa kuwa na biashara ndogo na za kati takribani milioni tatu zinazochangia Pato la Taifa kwa asilimia 27. Sekta hiyo pia ni muhimu katika kufikia maendeleo endelevu nchini ikichangia katika ajira na ubunifu.

Mteja anaweza kupata huduma hiyo kupitia tawi lolote la Benki ya Mwanga Hakika nchini. 

Ili kuipa thamani zaidi, benki hiyo imekuja na huduma ya ziada ya akaunti ya malengo (Fulsa saving account) itakayowawezesha wafanyabiashara wadogo kutunza fedha kwa malengo ya baadaye.