BRELA yataka wenye viwanda vidogo kujisajili watambulike

By Restuta James , Nipashe
Published at 10:11 AM Jun 21 2024
Mkurugenzi wa Leseni wa wakala huo, Andrew Mkapa.
Picha: Mpigapicha Wetu
Mkurugenzi wa Leseni wa wakala huo, Andrew Mkapa.

WAKALA wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA) umewataka wenye viwanda vidogo na vya kati kujisajili ili watambulike kitaifa na kimataifa na kufikia masoko makubwa, huku gharama ya kutimiza takwa hilo la kisheria ikianzia Sh. 10,000 inayolipwa mara moja katika uhai wote wa kiwanda.

Akizungumza wakati wa mafunzo ya waandishi wa habari mjini hapa jana yaliyoandaliwa na BRELA, Mkurugenzi wa Leseni wa wakala huo, Andrew Mkapa, alisema watu wengi wanakosa fursa za kuyafikia masoko makubwa yanayotokana na makubaliano ya kimataifa yanayoingiwa na nchi kwenye jumuiya za kikanda na kimataifa kutokana na kutokujisajili.

Alisema Sheria ya Taifa ya Usajili na Leseni za Viwanda, Sura ya 46, imeweka viwanda katika makundi mawili ya vikubwa na vya kati na vidogo.

Alisema kwa mujibu wa sheria hiyo, viwanda vikubwa na vya kati vinapewa leseni wakati vile vidogo vinapewa usajili.

Mkapa alisema ada ya leseni na usajili inalipwa mara moja na kwamba mmiliki hatozwi tena kwa muda wote wa uwekezaji.

Alisema tozo za BRELA kwa viwanda vyenye mtaji usiozidi Sh. milioni tano ni Sh. 10,000 wakati mtaji usiozidi Sh. milioni 10 ni Sh. 50,000.

"Cheti cha usajili kwa viwanda vidogo vyenye mtaji usiozidi Sh. milioni 100, ni cha kudumu na kinalipiwa mara moja tu… kadhalika viwanda vikubwa vyenye mtaji unaozidi kiasi hicho vinalipia leseni ambayo ni Sh. 800,000 nayo inalipwa mara moja pekee,” alisema.

Mkapa alisema kuwa baada ya kusajiliwa na kupewa leseni, wenye viwanda wanapaswa kuwasilisha taarifa kwa msajili kila mwaka bila gharama.

"Uhusiano na mikataba ya kimataifa ambao nchi inaingia unafungua masoko kama vile Soko Huru la Biashara Afrika (AfCFTA), soko la Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) na kwingineko. Usipojisajili ni vigumu kuwa na vigezo vya kufikia masoko makubwa na kukua,” alisema.

Ofisa huyo alisema masharti ya leseni na usajili wa viwanda ni rahisi kwa kuwa hakuna tozo za mwaka; badala yake ni taarifa zinazoainisha changamoto na mafanikio kila mwaka kwa ajili ya serikali kuweka kumbukumbu za huduma na bidhaa zinazozalishwa nchini na kuwezesha kutunga sera nzuri.

Kwa mujibu wa Mkapa, viambatanisho vya kusajili kiwanda ni pamoja na andiko la mradi, uthibitisho wa eneo kilipo na kibali cha Baraza la Taifa la Hifadhi Mazingira (NEMC).

Mkuu wa Kampuni katika Kurugenzi ya Kampuni na Majina ya Biashara BRELA, Lameck Nyangi, aliwataka wavumbuzi kujisajili ili kulinda kazi pamoja na majina yao ya biashara.