MDHIBITI na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali Zanzibar, Dk. Othaman Abassi Ali, amesema katika ukaguzi wake kwa mwaka wa fedha 2023 katika Benki ya Serikali ya Watu wa Zanzibar (PBZ), amebaini kasoro za kutozingatiwa kwa matakwa ya kisheria katika utoaji wa mikopo.
Akiwasilisha ripoti yake mbele ya Rais wa Zanzibar hivi karibuni, katika viwanja vya Ikulu visiwani humo, alisema mikopo hiyo ilikuwa na thamani ya Sh. bilioni 1.04 ambayo walipewa wafanyakazi wake sita bila ya kuzingatia miongozo na sera za utoaji wa mikopo ya benki.
Alisema ukaguzi wake umebaini wakati wa utoaji wa mikopo hiyo waliopatiwa walikuwa hawajathibitishwa kazini kinyume na toleo la utumishi wa umma la Febuari 21, 2022.
Alisema dosari nyingine ni mkopo huo haukupata idhini ya bodi ya wakurugenzi wa benki hiyo jambo lililosababisha kukosekana kwa uhalali wa uidhinishwaji wa mikopo hiyo.
Alisema mikopo hiyo iliyotolewa haiendani na muda wa mkataba wa ajira za wanufaika hao na ajira za mkataba zilikuwa na ukomo wa miaka mitatu, lakini waliopatiwa wanufaika hao ilikuwa na ukomo wa urejeshwaji baina ya miaka mitano hadi saba kinyume na sera ya mikopo ya benki.
Alisema kwa mujibu wa sera ya mikopo ya mwaka 2023, iliweka ukomo ya kiwango cha uidhinishwaji wa mikopo kwa watumishi kwa kiwango cha thamani ya mkopo chenye thamani ya shilingi milioni 200 ambao utaidhinishwa na mkurugenzi mtendaji wa PBZ na endapo kiwango hicho kitazidi kwa mtumishi wa PBZ italazimika kuombwa ridhaa kwa bodi ya benki hiyo.
Alisema cha kustaabisha kwamba uongozi wa benki hiyo ulitoa mikopo kwa watumishi wawili yenye thamani ya zaidi ya shilingi milioni 200 kwa kila mtumishi mmoja bila ya kushirikishwa bodi wa wakurugenzi wa PBZ jambo ambalo ni kinyume na sera ya mikopo waliojiwekea.
Akizungumzia uwanja wa michezo Gombani Pemba, Dk Abbasi alisema katika ukaguzi wake umebaini kuwepo kwa dosari ya usimamizi duni wa mradi wa usimamizi wa mkataba, kukosekana kwa udhibiti wa ubora, kutofuatwa kwa sheria na kanuni na ununuzi.
Alisema pia dosari nyingine ni mipango duni na usanifu wa mradi na kutopekuliwa kwa rasimu ya mkataba na mwanasheria mkuu wa serikali kwa lengo la kutolewa maoni ya kisheria kwa mujibu wa sheria namba 11 ya ununuzi na uondoshaji wa mali ya umma ya mwaka 2016.
Hata hivyo, alisema katika kipengele cha usimamizi wa kifedha ukaguzi wake ulifanya tathmini juu ya uwepo wa ufanisi katika utoaji wa fedha zilizopangwa na kuidhinishwa kwa matumizi ya mradi, ufanisi wa udhibiti wa ndani wa kifedha na kuzingatia kanuni za kifedha zinazoongozwa na hali ya malipo kama ilivyooneshwa katika hati za mradi husika.
“Licha ya mradi huo kupangiwa jumla ya shilingi bilioni 2.8 kwa ajili ya ukarabati kumebainika kujitokeza kwa ongezeko la gharama za ziada ya shilingi bilioni 2.842 na kusababisha ukarabati huo kufikia shilingi bilioni 5.642 sawa na ongezeko la asilimia 101.5 jambo ambalo ni kinyume na sheria namba 11 ya ununuzi wa mali za umma ya mwaka 2016,” alisema.
Aidha, alisema pamoja na dosari hiyo, lakini pia ukaguzi wake umebaini kupewa kazi ya mkataba kwa mkandarasi ambaye hakuwa na sifa na vigezo na kanuni namba 85 kanuni ndogo ya tano ya kanuni ya manunuzi ya umma ya mwaka 2020 inaeleza kwamba taasisi ya ununuzi na uondoaji wa dhabuni itathmini sifa ya zabuni kwa mujibu wa vigezo na taratibu za kufuzu zikiwamo katika nyaraka za kabla ya kufuzu ikiwa zipo na katika nyaraka za zabuni au nyinginezo za kufanya zabuni au nukuu.
“Ukaguzi wangu ulifanya mapitio ya barua kutoka mamlaka ya ununuzi na uondoshwaji wa mali za umma kwenda kwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo ya tarehe 14 Machi 2020 kuhusu mapendekezo ya zabuni,” alisema.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED