CWT yataka waraka upandishaji vyeo kuharakishwa

By Thobias Mwanakatwe , Nipashe
Published at 04:13 PM May 20 2024
Mwenyekiti wa CWT Mkoa wa Singida, Hamisi Mtundua.
Picha: Maktaba
Mwenyekiti wa CWT Mkoa wa Singida, Hamisi Mtundua.

CHAMA cha Walimu Tanzania (CWT) kimeitaka serikali kuharakisha mchakato wa kutoa waraka wa kupandishwa vyeo watumishi wa umma.

Mwenyekiti wa CWT Mkoa wa Singida, Hamisi Mtundua, amesema hayo jana wakati wa Mkutano Mkuu wa Umoja wa Walimu Kanda ya Kati na Kaskazini (NOCETEC), ambao uliwajumuisha walimu na viongozi wa CWT kutoka mikoa ya Tanga, Kilimanjaro, Arusha, Manyara, Dodoma na Singida ambao umefanyika mjini Singida.

"Walimu hawa ili waendelee kuwa na nyuso za furaha ni lazima wapewe kile wanachostahili kukipata, mpaka sasa tulitakiwa tuwe tumepewa waraka wa kupandishwa vyeo lakini hadi sasa hatujapata na kwa mujibu wa taratibu cheo kinapaswa kupanda Julai Mosi lakini tumecheleweshewa," amesema.

Mtundua amesema suala la kikokotoo bado walimu hawajamalizana na serikali na kwamba wana imani kubwa na serikali italifanyia kazi suala hilo, kwa kuwa kile wanachokipata walimu hakitoshelezi.

Naye Rais wa CWT, Leah Ulaya, amesema walimu wana kauli mbiu yao inayoitwa ‘wajibu na haki’ ambayo ili kutimiza wajibu wao ni lazima kuwa na viongozi mahiri.

"Ili tuweze kutimiza wajibu wetu kuna mambo matatu ya kuzingatia ambayo ni, mosi, kuwe na uhusiano wa kati ya pande mbili yaani mwajiri na mwajiriwa na yawe mahusiano mazuri ambayo yatafanya daraja kati ya mwajiriwa na ofisa utumishi," amesema Ulaya.

Amesema kuwa walimu wanatamani kuona mambo yao yote wanayohitaji wayapate kwa wakati na pia kuwepo kwa mshikamano baina yao na serikali.

Naye Katibu wa CWT Mkoa wa Singida, Digna Nyaki, akisoma risala ya walimu kwa mgeni rasmi amesema walimu wengi bado hawajalipwa madeni yao licha ya kwamba yamehakikiwa tangu mwaka 2017.

Pia amesema tatizo lingine linalowakabili ni walimu ambao wamepandishwa madaraja hawajapewa madaraja yanayostahiki na hakuna vifaa vya kufundishia baada ya kufanyika kwa mabadiliko ya mtaala wa elimu.

Akifungua mkutano huo, Mkuu wa Mkoa wa Singida, Halima Dendego amewaagiza wakurugenzi wa halmashauri na wakuu wa wilaya kutokalia madai ya watumishi muda mrefu badala yake wayafanyie kazi.