Dk. Biteko aishukia TGDC kushindwa kuchoronga visima

By Augusta Njoji , Nipashe
Published at 06:25 AM Apr 18 2024
Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk. Doto Biteko.
Picha: Maktaba
Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk. Doto Biteko.

NAIBU Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk. Doto Biteko ameinyooshea kidole Kampuni ya Uendelezaji Jotoardhi Tanzania (TGDC) kutokana kusuasua kuanza kuchoronga visima vya jotoardhi katika eneo la Ngozi mkoani Mbeya.

Akifungua Maonesho ya Wiki ya Nishati bungeni juzi, Dk. Biteko alisema TGDC ni miongoni mwa kampuni tanzu za Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) ambapo Aprili Mosi, 2024 ilitoa ahadi ya kuanza kazi hiyo lakini hadi sasa hawajaanza.

 “TGDC nimewawashia taa ya tahadhari, nilipokwenda Mbeya waliniambia wanaanza kuchoronga Aprili mosi mwaka huu kwa ajili ya kupata geothermal ili kupata umeme, naomba Katibu Mkuu tupia jicho kasi iongezeke,”alisema.

Alisema kwa sasa kuna umeme wa kutosha, lakini tatizo la kukatika linatokana na uchakavu wa miundombinu na kwamba serikali imejipanga kuifanya TANESCO kuwa na jina zuri kwa jamii ili iondokane na mtazamo hasi kwamba kila umeme giza likitokea au umeme ukikatika tatizo ni wao.

Kadhalika, alipongeza utendaji wa TANESCO kwamba wanafanya kazi nzuri usiku na mchana kuhakikisha wananchi wanapata huduma ya umeme.

Dk. Biteko alisema kutokana na kuwapo na umeme wa kutosha hata kituo cha umeme cha Kinyerezi megawati 150 hakijawashwa na kueleza kuwa hali hiyo imetokana na kuendelea kuwasha mashine za mradi wa umeme wa Bwawa la Mwalimu Nyerere.

Alisema mkakati mwingine wa Serikali ni kuhakikisha kwamba Tanzania inaunganishwa na nchi jirani ikiwamo Zambia, Uganda na Kenya.

Naibu Spika wa Bunge, Mussa Zungu alipongeza juhudi za serikali za kutatua tatizo la umeme na kwamba kwasasa makundi ya mitandao ya kijamii ya kukatika kwa umeme kwasasa hayazungumzii tatizo hilo.