Kamera ulinzi kuwekwa maeneo ya hoteli

By Rahma Suleiman , Nipashe
Published at 07:43 AM May 25 2024
Kamera za ulinzi.
Picha: Mtandaoni
Kamera za ulinzi.

WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa, Serikali za Mitaa na Idara Maalum za SMZ, Masoud Ali Mohamed, amesema serikali ya Zanzibar inakusudia kutekeleza mradi mkubwa wa kuweka miundombinu ya kamera za ulinzi katika maeneo yote ya ukanda wa hoteli za kitalii ili kudhibiti matukio ya uhalifu.

Aliyasema hayo jana katika kikao cha Baraza la Wawakilishi visiwani hapa wakati akijibu hoja za wajumbe wa baraza hilo waliochangia makadirio ya mapato na matumizi ya ofisi hiyo kwa mwaka wa fedha wa 2024/25.

Alisema kwa sasa serikali iko katika hatua za kufanya upembuzi yakinifu katika kutekeleza mradi huo muhimu ambao utalinda mali za wawekezaji katika hoteli za kitalii.

Kwa mujibu wa Waziri, jukumu la kuweka ulinzi ni pamoja na kuwahakikishia wawekezaji usalama wa miradi yao ni la serikali ndiyo maana uamuzi uliofikiwa ni kuja na mradi wa kuweka kamera za kudhibiti matukio ya uhalifu.

Aliyataja maeneo ambayo yatahusika na uwekaji wa miundombinu ya kamera za ulinzi ni Nungwi ambako kunaongoza kwa kuwapo kwa miradi mingi ya hoteli za kitalii.

Maeneo mengine ni Kiwengwa, Pwani Mchangani na mkoa wa Kusini Unguja ambako kasi ya ujenzi wa miradi ya hoteli za kitalii inaendelea.

“Mheshimiwa Spika, napenda niwajulishe wajumbe wa Baraza la Wawakilishi kwamba nia ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ni kuweka kamera za ulinzi katika ukanda wote wa miradi ya hoteli za kitalii kwa ajili ya kudhibiti matukio ya uhalifu,” alisema.

Hata hivyo alisema serikali imeanza kuchukua hatua za kukabiliana na matukio ya uhalifu ikiwamo kuanzisha kikosi cha polisi wa utalii ambacho kinafanya kazi katika maeneo yote ya ukanda wa hoteli za kitalii.

Alisema kwa kiasi kikubwa kikosi hicho kimefanikiwa kudhibiti matukio madogo yaliyokuwa yakijitokeza yakiwamo ya uporaji wa mali za watalii na vifaa vyao kama kamera.

“Mheshimiwa Spika kwa kiasi kikubwa tumefanikiwa kudhibiti matukio ya uhalifu ikiwamo watalii kunyang’anywa vitu vyao kwa kuja na kikosi cha polisi utalii ambacho kimesaidia kwa kiasi kikubwa,” alisema.