Kanuni mpya rufani ununuzi wa umma zaiva

By Renatha Msungu , Nipashe
Published at 06:52 AM May 24 2024
Katibu Mtendaji wa PPAA, James Sando
Picha: Mpigapicha Wetu
Katibu Mtendaji wa PPAA, James Sando

MAMLAKA ya Rufani ya Zabuni za Umma (PPAA) imepanga kuanza kutumia Kanuni za Rufani za Ununuzi wa Umma Julai Mosi, mwaka huu.

Aidha, mamlaka itatumia mfumo wa kuwasilisha malalamiko na rufani zitokanazo na michakato ya ununuzi wa umma lengo likiwa ni kuboresha eneo hilo.
 
Katibu Mtendaji wa PPAA, James Sando, alibainisha hayo jana jijini hapa wakati wa kikao kazi cha kupokea maoni ya uandaaji wa Kanuni za Rufani za Ununuzi wa Umma za Mwaka 2024 katika utekelezaji wa  Sheria ya Ununuzi wa Umma ya Mwaka 2023. 
 
Sando alisema Sheria Na.10 ya Ununuzi wa Umma ilitungwa na kupitishwa na bunge Septemba, 2023 na kwamba ili itumike vizuri, inategemea kanuni za ununuzi ambazo ziko katika hatua mbalimbali na zitakamilika na kuanza kutumika rasmi mwaka ujao wa fedha. 
 
"Sheria iko tayari lakini haiwezi kutumika bila kuwa na kanuni ndiyo maana tupo hapa kwa ajili ya kupokea maoni ya wadau wa ununuzi kuhusu Kanuni za Rufani za Ununuzi wa Umma za Mwaka 2024 ili kuiwezesha Sheria ya Ununuzi Umma ya Mwaka 2023," alisema Sando.
 
Aliongeza kuwa anaamini sheria hizo, zitapunguza changamoto kwenye rufani za ununuzi zilizokuwapo awali ambazo zilikuwa zinalalamikiwa na wazabuni.
 
Alisema baada ya kikao kazi kilichowakutanisha wadau wa ununuzi kutoka taasisi za umma, PPAA itaandaa kikao kingine na wazabuni ili nao watoe maoni yao kuhusu Kanuni za Rufani za Ununuzi wa Umma za Mwaka 2024 kabla ya sheria hiyo kuanza kutumika rasmi.
 
Kamishna wa Sera ya Ununuzi wa Umma kutoka Wizara ya Fedha, Dk. Frederick Mwakibinga, ambaye alimwakilisha Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Fedha, Jenifa Omolo, alisema serikali imefanya maboresho makubwa katika sheria hizo, hivyo watu watarajie mageuzi makubwa.
 
Dk. Mwakibinga alisema baada ya kanuni kukamilika, zitasaidia wananchi hususani wazabuni na wadau wa ununuzi kwenda kutumia kanuni ambazo zimekamilika na kuboreshwa na kuisaidia serikali kupata thamani halisi ya fedha katika miradi mbalimbali.
 
Alisema Sheria ya Ununuzi wa Umma Na. 10 ya mwaka 2023 imeboresha masuala mbalimbali ikiwamo kupunguzwa kwa muda wa kushughulikia malalamiko na rufani zinazotokana na michakato ya ununuzi wa umma. 
 
“Mfano, muda wa siku saba za kazi kwa ajili ya kusubiri malalamiko ya wazabuni (cool off period) kabla ya kutoa tuzo umepunguzwa na kuwa siku tano za kazi. Muda huo hautajumuisha njia za ununuzi ambazo hazihitaji ushindani kama vile ‘single source’, ‘minor value procurement’ na ‘shopping’.

“kadhalika muda wa ofisa masuhuli kushughulikia malalamiko ya zabuni umepunguzwa kutoka siku saba za kazi hadi siku tano za kazi pale ambapo hataunda jopo,” alisema Dk. Mwakibinga
 
Aidha, Dk. Mwakibinga alisema kutokana na maboresho hayo, endapo ofisa masuhuli ataunda jopo la mapitio ya malalamiko, atakuwa na siku saba za kazi na atatakiwa kuwajulisha washiriki wote wa zabuni juu ya uundwaji wa jopo hilo. Sambamba na hilo, alisema muda wa PPAA kushughulikia malalamiko au rufani umepunguzwa kutoka siku 45 hadi 40.
 
“Ili kuwezesha utekelezaji wa Sheria Mpya ya Ununuzi wa Umma ya Mwaka 2023, PPAA iko katika mchakato wa kuandaa Kanuni za Rufani za Ununuzi wa Umma za mwaka 2024. Pamoja na mambo mengine, kanuni hizo zitatoa wigo mpana wa kuwasilisha malalamiko. Mabadiliko hayo yatawapa wazabuni fursa ya kushindana kwa haki na uwazi katika zabuni mbalimbali,” alisema.