‘Majiji, miji hutumia gharama kubwa ulipaji fidia’

By Augusta Njoji , Nipashe
Published at 06:22 AM Apr 20 2024
Naibu Waziri ya Ujenzi, Godfrey Kasekenya.
Picha: Maktaba
Naibu Waziri ya Ujenzi, Godfrey Kasekenya.

TATHMINI ya awali ya gharama inayohitajika kulipa fidia kwa mali zilizomo ndani ya eneo la hifadhi ya barabara inapoongezwa ukubwa imeonyesha kuwa gharama kubwa zipo katika majiji na miji.

Naibu Waziri ya Ujenzi, Godfrey Kasekenya, aliyasema hayo bungeni jana alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Kibaha Vijijini (CCM), Michael Mwakamo.

Mbunge huyo alihoji kuhusu mpango wa serikali kuepuka mzigo mkubwa wa ulipaji wa fidia wakati inapoongeza ukubwa wa barabara.

Akijibu, Kasekenya alisema wizara hiyo kupitia Wakala wa Barabara nchini (TANROADS) imefanya tathmini ya awali ya gharama inayohitajika kwa ajili ya kulipa fidia kwa mali zilizomo ndani ya eneo la hifadhi ya barabara lililoongezwa la mita 7.5 kila upande na kuonesha kuwa gharama kubwa za fidia ziko katika majiji na miji.

Alisema serikali inaangalia uwezekano wa kuchepusha barabara kwenye maeneo hayo.

Aidha, alisema uchambuzi wa kina unafanyika ili kubaini ni barabara zipi zinahitaji upana wa eneo la hifadhi ya barabara wa mita 60 kwa kuzingatia mahitaji ya sasa na ya hapo baadaye ya kuzipanua kulingana na ongezeko la wingi wa magari na kazi hiyo itakapokamilika taarifa kamili itatolewa.

Awali, alifafanua kuwa serikali kupitia Sheria ya Barabara namba 13 ya mwaka 2007, iliongeza upana wa hifadhi ya barabara kutoka mita 45 hadi mita 60 kwa barabara kuu na za mikoa ili kukidhi mahitaji ya uendeshaji wa miundombinu ya barabara kwa wakati huu na wakati wa baadaye ili uendane na ongezeko la watu na ukuaji wa shughuli za kiuchumi.