Makonda kufanya kikao na mabalozi ili kuvutia watalii

By Beatrice Shayo , Nipashe
Published at 06:09 AM Apr 18 2024
Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Paul Makonda.
Picha: Maktaba
Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Paul Makonda.

MKUU wa Mkoa wa Arusha, Paul Makonda, amesema anatarajia kufanya kikao kwa njia ya mtandao na mabalozi wa Tanzania waliopo nje ya nchi, ili kuangalia namna ya kutangaza fursa za utalii imkoani hapa, kuwavutia watalii wengi zaidi.

Alitoa kauli hiyo alipokutana na Balozi wa Tanzania nchini Ujerumani, Hassan Mwameta na Balozi wa Tanzania nchini Ubelgiji, Jestas Nyamanga, waliofika ofisini kwake kuzungumza naye kuhusu fursa zilizopo katika utalii.

 "Mabalozi hawa ambao wanatuwakilisha katika taifa hili wanauzoefu, uelewa mpana kuhusiana na utalii wanaijua saiklojia ya mgeni atakapokuja katika nchi yetu na wanapata mrejesho wa mambo gani watalii wanayoyataka wanapokuja katika utalii," alisema.

Alisema atakapopata nafasi ya kufanya kikao na mabalozi hao watamweleza ni mambo gani ya kuwekewa mkazo ili kuhakikisha kuwa Tanzania inakuwa chachu ya chanzo ya kuwaleta watalii wengi.

Alisema mabalozi wamemuonyesha fursa zilizopo wao kama mkoa watachukua hatua kwa kuzikimbilia ili kuongeza watalii wengi mkoani Arusha.

Makonda alisema moja ya jambo ambalo linaingiza mapato kwa mkoa wa Arusha ni utalii, hivyo kila mmoja atatakiwa kupatiwa elimu ya utalii kwa upana ili kuongeza uchumi.

Alisema wataendelea kuboresha miundombinu ili kuhakikisha wageni wanapofika hawapati shida na suala la ulinzi litakuwa kipaumbele.

Makonda alisema wanataka kuwa na 'code' yaani mgeni akifika uwanja wa ndege kama mwenyeji umeenda kumpokea unakuwa na code yake atakapocheki inamuonyesha ni mtu sahihi anatambulika na serikali.

Mabalozi hao wamemueleza Makonda kuhusu fursa mbalimbali zinazopatikana kwenye nchi wanazoiwakilisha Tanzania na kuahidi kumpatia ushirikiano mkubwa katika kutangaza na kuvutia watalii ili wawekezaji kuja kutembelea mkoani Arusha na maeneo mengine yenye vivutio vya utalii.