WANANCHI wilayani Missenyi, mkoani Kagera wametakiwa kufichua wamiliki wa taasisi za kukopesha fedha zisizo rasmi ili serikali ichukue hatua kali dhidi yao na kuzuia wengi kuumizwa na mikopo isiyofuata taratibu za kisheria.
Rai hiyo ilitolewa mwishoni mwa wiki na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Missenyi, John Wanga, ambaye aliambatana na timu ya wataalamu wa Wizara ya Fedha wanaoendelea kutoa elimu ya fedha kwa wananchi mkoani Kagera.
Tayari timu hiyo imetembelea wilaya nne za mkoa huo ambazo ni Bukoba, Missenyi, Muleba na Biharamulo ambako ilifanya mikutano ya kuelimisha wananchi namna ya kutambua wakopeshaji halali na hatua wanazotakiwa kuchukua wanapokutana na mkopeshaji ambaye hafuati matakwa ya kisheria.
"Sisi viongozi wa serikali tunatakiwa tuendelee kushirikiana na wananchi kuwakemea watoa huduma wasio na nia njema kwa taifa wanaojali maslahi yao binafsi huku wakiwaumiza wananchi," alisema Wanga.
Alisema serikali haitasita kuwachukulia hatua watu wote watakaobainika kwenda kinyume cha maelekezo waliyopewa na Benki Kuu ya Tanzania (BoT) kabla hawajapatiwa leseni ya kuendesha shughuli za utoaji mikopo.
Ofisa Maendeleo ya Jamii Halmashauri ya Wilaya ya Missenyi, Flavian Nturwa, alisema ni wajibu wa waratibu wote wa huduma ndogo za fedha kuhakikisha wanatoa elimu kwa wananchi katika ngazi zote ili wawe na uelewa mpana wa masuala ya fedha.
"Tutahakikisha tunafanya mikutano ya mara kwa mara kwa wananchi wa pande zote, watoa mikopo na wapokeaji, ili wawe na uelewa wa pamoja hususan elimu ya mikataba kuepuka kusaini mikataba yenye masharti magumu," alisema Nturwa.
Mtoa Huduma za Mikopo, Salehe Hamisi alisema elimu itolewe juu ya utaratibu wa kusajili taasisi za fedha ili wafanyabiashara wajisajili kwa wingi na kutambulika rasmi.
Ofisa Usimamizi wa Fedha Idara ya Uendelezaji Sekta ya Fedha Wizara ya Fedha, Mary Mihigo, alisema ni muhimu kila mmoja kuwa na nidhamu ya fedha ili kufikia malengo na kurejesha mkopo aliochukua.
Wizara ya Fedha inaendelea kutoa elimu juu ya huduma ndogo za fedha ikiwa ni utekelezaji wa maagizo ya Rais Samia Suluhu Hassan ya kuhakikisha kila mwananchi anafikiwa na elimu ya huduma ndogo za fedha kuepuka 'mikopo umiza'
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED