Mwinyi asema utalii kichocheo uchumi usafiri wa anga

By Rahma Suleiman , Nipashe
Published at 11:41 AM May 16 2024

Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Ali Mwinyi.
Picha: Mpigapicha Wetu
Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Ali Mwinyi.

RAIS wa Zanzibar, Dk Hussein Ali Mwinyi, amesema utalii ni muhimu kwa mikakati ya maendeleo ya uchumi wa nchi na usafiri wa anga ndio kichocheo kikuu cha ukuaji wa uchumi huo.

Aliyasema hayo jana wakati akifungua kongamano la kimataifa la masuala ya anga la Jumuiya ya Afrika Mashariki lililofanyika visiwani Zanzibar na kuwashirikisha washiriki zaidi ya 200 kutoka nchi mbalimbali ikiwamo Uganda, Afrika Kusini, Sudan, Burundi, Somalia, Ethiopia na Kenya.

Dk. Mwinyi alisema, Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inazingatia mikataba yote ya usafiri wa anga ya kimataifa ili kuhakikisha ukuaji wa sekta hiyo unaendelea kuwa salama.

“Nchi yetu inajivunia mafanikio ambayo yamefikiwa katika sekta ya usafiri wa anga. Nachukua fursa hii kuwataka wadau na washirika wa usafiri wa anga kuimarisha ushirikiano ili kuhakikisha sekta hiyo inaendelea kukua kwa usalama,” alisema.

Alitaja baadhi ya mafanikio yaliyopatikana kuwa Tanzania imeendelea kushirikiana na nchi washirika chini ya mwavuli wa Taasisi ya udhibiti wa usalama wa usafiri wa Anga ya Jumuiya ya Afrika Mashariki, katika kuoanisha kanuni za usafiri wa anga ndani ya ukanda huo kwa lengo la kuwianisha taratibu, kuimarisha usalama na kuongeza ufanisi.

Alisema pia Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupata asilimia 87 ya usalama na ufanisi, mpango wa kimataifa wa ukaguzi wa usalama wa kimataifa uliofanywa na Shirika la Kimataifa la Usafiri wa Anga (ICAO) mwaka jana, ni kukuza usalama wa usafiri wa anga duniani kupitia ukaguzi na ufuatiliaji wa mara kwa mara wa nchi wanachama.

Aidha alisema mafanikio mengine ni uboreshaji wa mradi wa masafa ya mbali (VHF) unaojumuisha pia ufungaji wa vituo 18 vipya na redio katika viwanja vya ndege 12, na uwekaji wa mifumo ya kinasa sauti katika viwanja vinne vya ndege.

“Uwekaji wa mfumo wa Kutua kwa Ndege (ILS) katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Abeid Aman Karume ni ushahidi wa wazi kuhusu nia yetu ya kufanya usafiri wa anga kuwa salama na hivyo kuwa mwezeshaji wa sekta ya utalii ambayo, kama nilivyosema awali, ni muhimu kwa maendeleo ya Taifa letu,” alisema Dk. Mwinyi.

Aliwataka washiriki wa kongamano hilo kujadili na kutoa mapendekezo sio tu jinsi changamoto zilizoainishwa katika maeneo hayo zinavyoweza kutatuliwa, bali pia kubainisha jinsi fursa zinazohusiana na maeneo hayo zinavyoweza kutumika kikamilifu kwa manufaa ya usalama wa anga, uwezo, ufanisi na ulinzi wa mazingira katika Ukanda wa nchi zetu za Afrika Mashariki.

Alizishukuru nchi  Wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki na Bodi ya Taasisi ya Udhibiti wa Usalama wa Usafiri wa Anga ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC CASSOA) kwa kuipa nafasi Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya kuandaa kongamano hilo.

Alisema moja ya malengo ya CASSOA ni kusaidia nchi wanachama katika kutimiza majukumu yao ya udhibiti wa usalama chini ya Mkataba wa Jumuiya ya Afrika Mashariki na Mkataba wa Chicago.

Pia, alisema nchi inaendelea kunufaika na uhusiano mzuri wa kufanya kazi na nchi zote Wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki unaozingatia dira ya pamoja na uelewa wa kina kwa madhumuni ya usalama wa anga na kwa maendeleo ya Mataifa hayo.

Waziri wa Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi, Dk. Khalid Salum Mohammed, alisema watu wengi wanafikiria usafiri wa anga ni salama na haraka hivyo ni muhimu wadau wakawa na uwelewa wa kutosha juu ya mada ya usalama ambayo itazungumziwa katika kongamano hilo.

Alisema suala la usalama sio la kupuuziwa na abiria wanaosafiri matarajio yao ni kufika salama na wanapopata msukosuko abiria huingia na taharuki.

Spika wa Bunge la Afrika Mashariki, Joseph Ntakiruimana na Mwenyekiti wa Jumuiya ya Afrika Mashariki masuala ya anga, Hamza Johari, walisema wameanzisha jumuiya ya anga ili kusaidia katika kukuza uchumi na kuwa endelevu na kuleta maendeleo ya kichumi na kuwa chachu ya maendeleo katika taifa.

Kaulimbiu ya kongamano hilo la sita la Jumuiya ya Afrika Mashariki la Usafiri wa Anga ni “Mustakabali wa Usafiri wa Anga: Kudumisha Mifumo ya Usafiri wa Anga yenye Ustahimilivu, Uendelevu, Ubunifu na Usalama".