Polisi wajibebesha jukumu kuelimisha utapeli wa fedha

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 10:20 AM May 28 2024
Mkaguzi wa Polisi Wilaya ya Missenyi, Baraka Mafwimbo.
Picha: Maktaba
Mkaguzi wa Polisi Wilaya ya Missenyi, Baraka Mafwimbo.

MKUU wa Polisi Wilaya ya Missenyi mkoani Kagera, Jonas Soa, amasema kuwa ni wajibu wa polisi kuelimisha wananchi kuhusu mbinu zinazotumiwa na matapeli kujipatia fedha.

Aidha, amesema kuna umuhimu wa kuwaeleimisha polisi jamii juu ya fedha kwa kuwa wanaishi nao kwenye maeneo yao ambayo itasaidia kupunguza matukio ya watu kutapeliwa.

Pia, ameahidi kutoa ushirikianokwa timu ya wataalam wa Wizara ya Fedha ambao wanafanya kampeni ya kutoa elimu ya feda kwa umma katika mikoa mbalimbali nchini.

Aliyasema hayo wakati akizungumza na askari polisi katika semina ya masuala ya fedha iliyofanyika katika Kituo cha Polisi Kyaka, pamoja na mambo mengine alisema wataendelea kuwaelimisha polisi wengine ambao hawajafikiwa na elimu hiyo. 

Alisema kuwa elimu ikiwafikia wananchi wote nchini itaisaidia serikali kupunguza migogoro ya kesi mbalimbali zinazoendelea kwenye vituo vya polisi kuhusu mikopo inayowakumba wananchi mbalimbali.

Mkaguzi wa Polisi Wilaya ya Missenyi, Baraka Mafwimbo, aliiomba serikali kuongeza nguvu ya kudhibiti na kuimarisha mifumo ya taasisi zinazohusika na utunzaji wa taarifa binafsi za wananchi, kuhakikisha zinalinda taarifa hizo, ili kuepusha taarifa hizo kufikiwa na watoa huduma ya mikopo na kuweza kuwashawishi kukopa fedha.

“Binafsi nimewahi kupigiwa simu na kushawishiwa kuchukua mkopo na watoa huduma ambao sikujua taarifa zangu wamezitoa wapi, lakini walikuwa wananielezea kama wananifahamu, hawakuweza kufanikiwa  kwa kuwa nimewahi kupata elimu ya masuala ya fedha zamani,” alisema Mafwimbo.

Ofisa Usimamizi wa Fedha Idara ya Uendelezaji Sekta ya Fedha Wizara ya Fedha, Mary Mihigo, alisema ni muhimu wananchi wakajua kuwa wanapaswa kuomba mikopo kwa taasisi zilizosajiliwa rasmi kuepusha matapeli.

“Utajua kuwa ni taasisi rasmi ya kukopesha, kupitia tovuti ya Benki Kuu ya Tanzania  (BoT), ambayo imeorodhesha taasisi rasmi zote za utoaji mikopo nchini, hivyo ni lazima mwananchi kabla hajakopa kujiridhisha kwenye usajili wa taasisi  husika,”alisema Mihigo. 

Alisema kuwa Wizara ya Fedha, itaendelea kutoa elimu ya masuala fedha kwa wananchi wa makundi mbalimbali, ili kuhakikisha wanakuwa na uelewa mpana wa masuala ya fedha ikiwemo elimu ya mikataba, uwekezaji na mikopo umiza.