Serikali yataka huduma za kifedha kufika vijijni

By Faustine Feliciane , Nipashe
Published at 11:08 PM May 27 2024
Waziri Ofisi ya Rais, Uwekezaji na Mipango, Profesa Kitila Mkumbo (kushoto) akizungumza na Mkurugenzi Mtendaji kundi la Makampuni ya Craft Silicon, Kamala Budhabhati (kulia), katikati ni Mtendaji Mkuu wa Kampuni nchini Tanzania, Mili Rughani.
Picha: Faustine Felician
Waziri Ofisi ya Rais, Uwekezaji na Mipango, Profesa Kitila Mkumbo (kushoto) akizungumza na Mkurugenzi Mtendaji kundi la Makampuni ya Craft Silicon, Kamala Budhabhati (kulia), katikati ni Mtendaji Mkuu wa Kampuni nchini Tanzania, Mili Rughani.

SERIKALI imezitaka taasisi za kifedha kuelekeza nguvu zao kupeleka huduma hizo kwenye maeneo ya vijijini yenye mahitaji zaidi.

Akizungumza jijini Dar es salaam mwishoni mwa wiki wakati akizindua kampuni mpya hapa nchini ya malipo kwa njia ya mtandano ya Craft Silicon, Waziri wa ofisi ya Rais, Uwekezaji na Mipango, Profesa Kitila Mkumbo, alisema kuwa mambo sasa yamebadilika na dunia inakwenda kidigitali hivyo ni lazima huduma za kifedha kwa njia ya mtandao zifike na vijijini.

Alisema vijana ndio kundi kubwa linalopaswa kuingia kwenye aina hiyo ya huduma za kifedha.

"Kama Serikali tuna fahamu umuhimu wa matumizi ya kidigitali, wito wetu kwa makampuni kama haya kuelekeza nguvu zao vijijini, huduma hizi zifike maeneo hayoambayo uhitaji ni mkubwa pia," alisema Profesa Mkumbo.

Alisema kwa sasa dunia ina hama kutoka mfumo wa kawaida uliozoeleka na kwenda kwenye mfumo wa kidigitali hivyo lazima watanzania nao waende sawa na kasi ya mabadiliko.

Aidha, alisema Serikali itaendelea kuweka mazingira mazuri kwa wawekezaji kuendelea kuja Tanzania na kuwekeza katika maeneo mbalimbali.

"Ujio wa kampuni hii ya kimataifa ya Craft Silicon  ni matunda ya kuwa na mazingira mazuri ya uwekezaji,Serikali inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan itaendelea kuboresha sera za uwekezaji na kuendelea kuwavuta wawekezaji wengi zaidi," alisema Profesa Mkumbo.

Aidha, Mkurugenzi Mtendaji wa kundi la makapuni la Craft Silicon, Kamal Budhabhati, alisema mazingira mazuri ya uwekezaji yamemshawishi kufungua ofisi yake hapa Tanzania.

Alisema kampuni hiyo ilinzishwa mwaka 2006 nchini India na ipo kwenye nchi 15 tofauti za Afrika.

"Tunaamini uwepo wetu kama kampuni ya malipokwa njia ya mitandao tutatoa ajira kwa watanzania, lakini pia kutoa huduma kwa wananchi wote, tunajipanga kuwafikiwa watu wengi zaidi," alisema Budhabhati.

Kwa upande wake Mkuu wa kampuni hiyo ofisi ya Tanzania, Mili Rughani, alisem wataendelea kuwekeza Tanzania na kutoa suluhisho la masuala ya malipo kwa njia ya mtandao.