Serikali yatoa maelekezo bei kwa nyumba za WHI

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 06:24 AM May 26 2024
Waziri Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, George Simbachawene.
Picha:Mpigapicha Wetu
Waziri Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, George Simbachawene.

SERIKALI imeiagiza Taasisi ya Watumishi Housing Investments (WHI) kufanya marejeo na kukokotoa upya bei ya kuuza nyumba zao zilizoko kijiji cha Isangijo, Kata ya Bukandwe, wilayani Magu, mkoani hapa, ili ziendane na kipato cha watu wa eneo hilo.

Waziri Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, George Simbachawene, alipotembelea mradi huo na alisema msingi mkubwa wa Watumishi Housing ni kujenga nyumba kwa ajili ya watumishi na ili kuendana na msingi huo, bei za kupangisha na kuuza nyumba ziwe rafiki.

Diwani wa Bukandwe, Marco Minzi, awali akidokeza sababu za watu kushindwa kuzichangamkia nyumba hizo ni gharama kuwa juu kulinganisha na hali ya uchumi wa watu wa eneo hilo, hivyo kuomba zipunguzwe.

Minzi alisema nyumba moja yenye vyumba vitatu, sebule, jiko na sehemu ya chakula inauzwa Sh. milioni 82, ambapo ni gharama kulinganisha na watu wa maeneo hayo.

Mkurugenzi Mtendaji wa Watumishi Housing, Dk. Fred Msemwa, alisema mradi huo ambao ni wa kwanza kutekelezwa kwa mwaka wa fedha 2015/16, ukihusisha ujenzi wa nyumba 59, kwa ajili ya kuziuza kwa watumishi wa umma wa kada zote, mpaka sasa zilizouzwa ni nyumba 20 na 39 zikibaki.

“Mradi huu ulikamilika mwaka 2018. Nyumba 20 zimeuzwa kwa Chuo cha Mipango kilichoko Dodoma ambacho kina kampasi yake hapa Mwanza. Nyumba 39 tumezipangisha kwa watumishi wa umma,” alisema.

Hata hivyo, Msemwa alisema wamepokea maombi ya kupunguza bei za nyumba hizo na kuahidi kufanya marejeo ili kukokotoa bei sawa na hali halisi ya kipato cha watu wa hapo.

Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Magu, Mohamed Ramadhani, alisema bado wana uhitaji mkubwa wa nyumba kwa ajili ya watumishi kulinganisha na idadi ya nyumba zilizoko.

Ramadhani alitaka Watumishi Housing kuongeza nyumba maeneo ya karibu na wanapofanyia kazi watumishi ili kuepusha usumbufu wa kuchelewa ofisini.

“Magu tuna watumishi 3,079, lakini si watumishi wote wana nyumba, kwa hiyo kuna mahitaji makubwa sana ya nyumba kwa ajili ya watumishi.

“Nyumba nyingi zinazopatikana zinaweza kuwa ama zipo mbali na kituo cha kazi au hazina staha na hadhi ya kukaa mtumishi,” alisema.

Ramadhani alisema wanatamani kuona miradi kama hiyo inakuwapo maeneo mengine kama makao makuu ya wilaya pamoja na karibu na hospitali ili watumishi wanafanya kazi kwa kupokezana mchana na usiku iwe rahisi kwao.