TANESCO yajivunia mifumo ya kidijiti

By Joseph Mwendapole , Nipashe
Published at 10:25 AM Jun 21 2024
 Ofisa huduma kwa wateja wa Shirika hilo, Fatuma Mohamed.
Picha: Mpigapicha Wetu
Ofisa huduma kwa wateja wa Shirika hilo, Fatuma Mohamed.

SHIRIKA la Umeme Tanzania (TANESCO), limesema huduma zake nyingi zinapatikana katika mifumo ya kidijiti hali iliyosaidia kuleta mageuzi makubwa ya utoaji wa huduma.

Uwekezaji huo ni sehemu ya utekelezaji wa maagizo ya Rais Samia Suluhu Hassan ya kuyataka mashirika ya umma yawekeze katika mifumo hiyo ya kidijiti.

Hayo yalisemwa jana na Ofisa huduma kwa wateja wa Shirika hilo, Fatuma Mohamed, wakati akizungumza na waandishi wa habari katika Maonyesho ya Wiki ya Utumishi wa Umma yanayofanyika jijini Dodoma.

 Alisema uwekezaji uliofanywa na shirika hilo kwenye mifumo ya TEHAMA umesaidia kwa kiwango kikubwa kuleta mageuzi kwenye utoaji wa huduma na kuwapunguzia gharama wateja.

Alisema TANESCO ambalo ni shirika la umma limejikita kutoa huduma katika mfumo wa kidijitali kuanzia kuunganisha umeme pamoja na kuongeza wigo katika matumizi ya TEHAMA kwa upande wa kutoa taarifa kwa jamii kuhusu shirika hilo.

“TANESCO limejikita pia katika kutoa huduma katika mfumo wa kidijitali tukianzia na mfumo wetu wa kuunganisha umeme wa NIKONECT, ambao ni wa kidijitali kwa sasa mteja siyo lazima afike ofisini ili kupata huduma ya kuunganishiwa umeme,” alisema.

“Mteja popote alipo akiwa na simu janja au hata akiwa na simu zile za kitochi anaweza kufanya maombi na anaweza kuunganishiwa umeme bila kufika ofisi za TANESCO,” alisisitiza.

Fatuma alisema shirika hilo limeongeza wigo wa kutumia TEHAMA kwa upande wa kutoa taarifa mbalimbali ambayo unaitwa JISOT na kupitia mfumo huo mteja anaweza akatoa taarifa kwa njia ya simu janja.

“Kwa kupitia namba yetu ile ile ya kutolea taarifa kwenye kituo cha miito ya simu TANESCO na kwa kweli tumeona mafanikio makubwa kwani wananchi wanahudumiwa kwa haraka wanapotoa taarifa zao,” alisema.

Alisema kwa kutumia JISOT taarifa hiyo inatumwa kupitia namba ya kutolea taarifa kwenye kituo cha miito ya simu Tanzania TANESCO ambayo namba hiyo pia inatumika kwa mtandao wa kijamii.

Aidha, alisema faida ya huduma hizo ni kuokoa muda wa mteja kusafiri umbali mrefu pamoja na usumbufu wa kutafuta ofisi, ili kujipatia huduma, lakini pia TANESCO wameweza kupata taarifa kwa haraka kiganjani na urahisi wa kuhudumia wateja kwa uharaka.

Fatuma alisema mfumo wa JISOT unamruhusu mteja kujihudumia mwenyewe kwa kuuliza maswali au kupitia changamoto atakazozipata kutokana na huduma au hitilafu ya umeme itakayojitokeza kwenye eneo lake.