Taratibu kuinyanyua Mv. Clarias zinaendelea

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 11:26 AM May 21 2024
Meli ya Mv. Clarias iliyozama ziwani.

KAMPUNI ya Huduma za Meli (MSCL) imesema wataalamu wanaendelea na utaratibu wa kuinua Meli ya Mv. Clarias inayohudumia katika Ziwa Victoria, iliyozama wakati imeegeshwa Bandari ya Mwanza Kaskazini.

Akielezea hatua zinazoendelea, Ofisa Uhusiano kwa Umma wa MSCL, Abdulrahman Salim Ally, alisema meli hiyo yenye uwezo wa kubeba abiria 216 na tani 10 za mizigo ilipinduka usiku wa kuamkia Jumapili majira ya saa 11 alfajiri na haikuwa na mali wala mtu.

Alisema hali hiyo ilizua taharuki kwa abiria na jamii wanaotegemea meli hiyo kwa ajili ya usafiri na usafirishaji wa mizigo, kwamba hadi sasa chanzo cha tukio hilo bado hakijajulikana.

Salim alisema uchunguzi kubaini chanzo cha ajali hiyo utaanza baada ya wataalam kukamilisha shughuli za kuinyanyua na kuipeleka kwenye chelezo, ambapo itafanyiwa marekebisho kwa matatizo yanayoweza kuwa yameikabili pale ilipoanguka.

"Hai hii imesababisha kusitishwa kwa safari za meli hiyo pamoja na meli nyingine ya Mv.Butiama inayofanya safari za Mwanza kwenda Ukerewe ambayo ilizibiwa eneo la kutokea," alisema Salim.

Baadhi ya abiria waliokosa huduma kutokana na meli hiyo kupinduka majini, akiwamo Flora Kila alisema ratiba yake imevurugika na kuingiwa na hofu juu ya hatima ya kufika anakokwenda.

Abiria mwingine Katwale Thomas aliiomba serikali kufanya uchunguzi wa kina juu ya tatizo hilo sambamba na kuvifanyia marekebisho, ili kujihakikishia usalama wa usafari.

Imeandikwa Na Remmy Moka, SAUT