TASAC yatoa gawio la Sh. bilioni 19.1 kwa mfuko wa hazina wa taifa

By Romana Mallya , Nipashe
Published at 04:08 PM Jun 13 2024
TASAC yatoa gawio la Sh. bilioni 19.1 kwa mfuko wa hazina wa taifa.
PIcha: Mpigapicha Wetu
TASAC yatoa gawio la Sh. bilioni 19.1 kwa mfuko wa hazina wa taifa.

SHIRIKA la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC) limetoa gawio la Sh. bilioni 19.1 kwa mfuko wa hazina wa taifa.

Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TASAC, Nahson Sigalla, amesema hayo mara baada ya shirika hilo kutoa gawio lake, fedha zilizopokewa na Rais Samia Suluhu Hassan.

Gawio hilo liliwasilishwa na Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi Mussa Mandia pamoja na Sigalla.

Sigalla amesema serikali imechagiza sekta ya usafiri majini na kuchangia matokeo ya ukusanyaji mzuri wa mapato kwao ambayo yamewezesha kutoa gawio la Sh. bilioni 19.1 kwa mfuko huo

“Tunaipongeza sana serikali kwa uongozi thabiti hasa katika sekta ya uchukuzi na kusababisha na sisi TASAC kuchangia katika mfuko huu wa hazina ya taifa Sh. bilioni 19.1 kama matokeo mazuri ya utekelezaji wa majukumu yetu,” amesema.

Msajili wa Hazina, Nehemiah Mchechu, amethibitisha kwamba, TASAC imetoa gawio hilo kwa mwaka unaoishia Juni 2024, huku akitoa shukrani za dhati kwa utendaji wao mzuri wa kazi.

Katika hafla hiyo, Rais Samia amesema hatokubali mtu yeyote amkwamishe kwenye azma yake ya kuleta mageuzi ya kiuchumi anayoendelea nayo na kwamba, kila mmoja akafanye mageuzi ili kuongeza tija katika kukuza uchumi.

“Hivi karibuni tumeingia tena kwenye kundi la uchumi wa kati kama ambavyo imeainishwa na wenzetu wa Benki ya Dunia (WB), sasa ili uendelee kubakia katika kundi hilo ni lazima kuwe na mageuzi makubwa katika uchumi ili kuendelea kuaminika zaidi,” amesisitiza.
Rais Samia amesisitiza agizo lake la kutaka mifumo ya serikali kusomana ifikapo mwezi Desemba, mwaka huu, bila kuwa na kisingizio chochote.