TRA yajivunia makusanyo kupaa miaka 3 ya Samia

By Peter Mkwavila , Nipashe
Published at 04:17 PM May 20 2024
Meneja wa TRA, Mwita Ayubu.
Picha: Maktaba
Meneja wa TRA, Mwita Ayubu.

MAMLAKA ya Mapato Tanzania (TRA) Mkoa wa Dodoma umeongeza wastani wa ukusanyaji kodi kutoka Sh.bilioni 15.19 hadi Sh.bilioni 18. 71 katika kipindi cha miaka mitatu ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan.

Akizungumza na waandishi wa habari kuhusu mafanikio ya mamlaka hiyo jijini hapa, Meneja wa TRA, Mwita Ayubu, amesema mafanikio hayo ya makusanyo yametokana na uboreshaji wa uhusiano kati yao na walipakodi.

Amesema kuwa mwaka 2021 Mkoa wa Dodoma ulikuwa na wafanyabiashara 3,812 wanaotumia mashine ya EFD, hivi sasa wameongezeka na kufikia 9,367 ikiwa ni ongezeko la wafanyabiashara 5,555.

“Mengine yaliyowezesha kupanda kwa kiasi hicho cha fedha cha ukusanyaji ni ongezeko la uwekezaji na ukuaji wa shughuli za kiuchumi ikiwamo uzalishaji viwanda na sekta za ujenzi na usafirishaji na uhamasishaji kwa kupitia elimu kwa mlipakodi,” amesema.

Amebainisha kuwa pia ongezeko la matumizi ya mifumo ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) katika usimamizi wa kodi kutoka kwa wananchi kwa kulipa kodi kwa hiari, kuongezeka kwa hamasa ya ulipaji kodi kutoka kwa wananchi kwa kuona matumizi sahihi ya kodi wanazolipa.

Hivyo, amewasisitiza wafanyabiashara kutumia mashine za EFD kutokana na kuwapo kwa faida kama vile uboreshaji wa kumbukumbu za biashara kwa njia za elektroniki ambayo ni salama na ya kuaminika.

Hata hivyo, amesema mamlaka hiyo inakabiliana na tatizo la kuongezeka kwa wimbi la matumizi ya stempu za kielektroniki za kughushi kwa walipakodi, hali inayosababisha upotevu mkubwa wa mapato.