Ummy azindua kampuni tanzu ya Bohari ya Dawa

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 10:50 AM Jun 21 2024
WAZIRI wa Afya, Ummy Mwalimu.
Picha: Mtandao
WAZIRI wa Afya, Ummy Mwalimu.

WAZIRI wa Afya, Ummy Mwalimu amezindua Kampuni Tanzu ya Bohari ya Dawa (MSD MEDIPHAM Manufacturing Co. Ltd), itakayosimamia viwanda vya kuzalisha bidhaa za afya, pamoja na kuzindua Bodi ya Usimamizi wa kampuni hiyo.

Aliisisitiza kampuni hiyo kushirikisha wabia watakaokuwa tayari kushirikiana na MEDIPHAM kuzalisha bidhaa za afya, na kuendelea kutoa kipaumbele wazalishaji wa ndani.

Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini ya MSD, Rosemary Silaa, alisema kuwa kuwa kampuni hiyo ni matokeo ya Sheria ya MSD kufanyiwa marekebisho mwaka 2021, na kuongezewa jukumu la kuzalisha bidhaa za afya na amewaelekeza wajumbe hao wa bodi kuandaa mpango mkakati wa kampuni hiyo, pamoja na mfumo wa kutathimini namna ya kufikia malengo watakayojiwekea.

Silaa alisema ana imani kuwa kampuni hiyo itafanikiwa, ikiwa na mikakati mizuri, akitoa mfano kuwa kiwanda cha barakoa kilianza mwaka 2021 na mtaji wa Sh. bilioni 1.6 na hadi sasa wameshapata faida ya Sh. bilioni 4.8.

Mkurugenzi Mkuu wa MSD, Mavere Tukai, amesema tayari kuna viwanda vitatu vinavyozalisha, ambavyo ni pamoja na viwili vya barakoa (surgical& N95) vilivyopo Keko na kiwanda cha mipira ya mikono cha Idofi, Makambako.

Viwanda vingine vilovyopo mbioni kuanzishwa, ni pamoja na cha dawa Zegereni, Kibaha na cha bidhaa za pamba mkoani Simiyu.

Tukai, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Bodi ya usimamizi wa Kampuni Tanzu (MSD MEDIPHAM), alisema kuwa jukumu lao kubwa ni kuhakikisha miradi yote iliyoanzishwa inaendelezwa na uendeshaji wake kuwa wenye tija