Waagizaji dawa watakiwa kuwa wazalendo, kufuata sheria

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 08:39 AM Apr 09 2024
Mganga Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Dk. Thomas Rutachunzibwa.
Picha: Maktaba
Mganga Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Dk. Thomas Rutachunzibwa.

WAAGIZAJI wa dawa wametakiwa kufanya kazi kwa ubora, kutanguliza uzalendo, kuzingatia sheria na taratibu zilizowekwa na Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA) ili dawa hizo ziweze kutumika katika matumizi yaliyokusudiwa.

Hayo yalibainishwa na Mganga Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Dk. Thomas Rutachunzibwa wakati wa warsha iliyowakutanisha wadau wa uagizaji wa dawa kutoka Kanda ya Ziwa iliyofanyika Jijini Mwanza.

Alisema baadhi ya waagizaji wa dawa siyo waaminifu wanatumia njia za panya na kutopitia TMDA kwa ukaguzi wa dawa hizo ili kubaini kama zinafaa kwa matumizi ya binadamu.

Aidha, aliwataka kutotanguliza fedha katika kutekeleza majukumu bali wajali afya za watu kwa kuagiza bidhaa zenye viwango vinavyokubalika.

Alisema serikaki imeimarisha udhibiti ubora wa dawa katika maeneo ya mipakani kwa kuhakikisha hakuna dawa zinazoingia kinyume na utaratibu, huku doria imara katika bandari zote na maneno ya viwanja vya ndege zimewekwa wakishirikiana na wahudumu wa afya katika maeneo hayo.

Mkurugenzi Udhibiti wa Dawa kutoka TMDA, Daktari Yonah Mwalwisi alisema wadau hao ni watu muhimu lakini ni vyema wakawauzia wananchi bidhaa tiba kwa kufuata masharti na sheria za kuuza na kuagiza bidhaa tiba, ili zitumike katika makusudi yaliyowekwa na mamlaka hiyo

Alisema: "Wapo baadhi ya watu wamekuwa wakitumia vibaya dawa za uzazi na zinginezo kwa matumizi yasiyo sahihi hasa wale wanaonunua kwa lengo la kutoa mimba  na kuwataka wauzaji wa dawa kutoa maelekezo stahiki kabla ya kuuza kwa wananchi kwa sababu dawa lazima itumike kwa lengo la kutibu na siyo vinginevyo".

Katibu wa Chama cha Waagizaji wa Dawa (TAPI), Abbas Mohammed ambaye alikuwa mmoja wa wadau wa warsha hiyo alisema mabadiliko ya teknolojia yanakwamisha shughuli nzima ya  uagizaji na usambaji wa dawa.

Alisema mchakato wa usajili wa dawa hauendani na kasi ya maendeleo na madaliko ya teknolojia ya sasa katika kuhudumia wananchi ipasavyo.

Hivyo aliiomba TMDA iweke mifumo mizuri na rafiki katika kuzuia mianya yote ya kuagiza na kuingiza dawa kwa njia isiyo halali kwani inakwamisha ufanisi wa kazi kwao.