Wadau 600 kushiriki maonyesho utalii

By Cynthia Mwilolezi , Nipashe
Published at 07:37 AM May 25 2024
 Mkurugenzi wa Kilifair Ltd, ambao ni waandaaji wa maonyesho hayo, Dominic Shoo
Picha: Mpigapicha Wetu
Mkurugenzi wa Kilifair Ltd, ambao ni waandaaji wa maonyesho hayo, Dominic Shoo

ZAIDI ya wanunuzi 600 wa utalii kutoka nchi 40 duniani na waonyeshaji pamoja na wadau 468 wa utalii kutoka nchi 37, wamethibitisha kushiriki maonyesho ya kimataifa ya Karibu -Kilifair yanayotarajiwa kuanza Juni 7 hadi 9, mwaka huu jijini Arusha.

Vilevile, wadau hao na wanunuzi  wa  utalii  watatembelea vivutio vya utalii, ili wakawe mabalozi wazuri kwenye nchi zao.

Akizungumza jana jijini Arusha, Mkurugenzi wa Kilifair Ltd, ambao ni waandaaji wa maonyesho hayo, Dominic Shoo, alisema lengo la maonyesho hayo ni kutangaza vivutio vilivyopo nchini na wakauze nchini kwao. 

"Siku hizi tatu tunatarajia kuwa na kiwango kikubwa cha biashra kwa sababu lengo letu kubwa  kukutanisha wadau toka mataifa mbalimbali duniani, kuja kujua vivutio vyetu hapa Tanzania, wavitembelee na kuweza kuwa mabalozi wazuri, kwa ajili ya kuuza vivutio vya Tanzania," alisema. 

Alisema mwaka huu onyesho hilo ni kubwa kuliko la mwaka jana, sababu  wamekua na waonyeshaji zaidi na mwamko wa  wanunuzi ni mkubwa kuliko mwaka jana na wamekua na kiwango cha juu, kuliko mwaka jana kutokana na vitu ambavyo wameweza kuvinunua, ili kuhakikisha onyesho hilo linalingana na hadhi ya viwango vya kimataifa. 

Aidha, alisema Juni,   8  watakuwa na tamasha la muziki utakaoleta watu pamoja na utakuwa wa kiwango cha kimataifa kutokana na kushirikisha wataalamu wa burudani. 

"Kwa sababu siku hizi tatu tumeona tutakuwa na wageni wengi Arusha, lakini hawana burudani ya kutosha tukaona  kuliko  wakapate burudani sehemu tofauti, ambazo hazina hadhi tumeamua kuwaandalia kitu kipya kitakachowapa burudani Juni nane mwaka huu,hapa hapa viwanja vya Magereza  na tumeunga na wataalamu wa burudani tunashirikiana nao," alisema. 

Hata hjvgo alisema utalii unakua na kwamba ambapo  msimu huu wa utalii umefunguka mapema ukilinganisha na mwaka jana, ina maana huhitaji wa kiu ya kwenda kwenye hifadhi  ni mkubwa. 

"Lakini   watu wana hoteli mpya nyingi na wanabishara mpya, wanataka juhakikisha wengi wanazijua na kupitia hapo wajue taarifa zao na bei zake,"alisema 

Kwa mujibu wa Shoo, maisha sasa hivi ni Afrika, ukienda nje ya nchi  onyesho lolote linalokosa Mtanzania wanashtuka, sababu Afrika nkombozi wao  Tanzania kwenye sekta ya utalii. 

Aliyataja baadhi ya mataifa hayo yafakayoshiriki knyesho hilo, kati ya 40 wanakotoka wanunuzi wa utalii kuwa ni  Ujerumani, Amerika, Italia, nchi za Afrika Mashariki, Aftika Kusini na  Asia.  

Maonyesho hayo yanatarajia kufunguliwa na Waziri wa Maliasili na Utalii, Angellah Kairuki. 

Mkuu wa kitengo  cha masoko na mauzo,  kutoka kampuni ya Media Works, Noel Petro, aliiomba serikali kuruhusu ujenzi wa  mabanda ya maonyesho ya kudumu, ili kuwepo kwa mazingira salama nyakati zote, badala ya kusubiri wakati wa onyesho tu. 

"Kutokana na maonyesho haya ni ya kipekee kwetu sisi, yanaleta fursa ya utalii kwani wateja wetu wakubwa zaidi ya asilimia 70  wanatokana na utalii."alisema.