Wahitimu SUA wapewa mchongo ajira

By Christina Haule , Nipashe
Published at 06:18 AM May 26 2024
Mwenyekiti wa Baraza la SUA, Jaji Mkuu Mstaafu Mohamed Chande Othman.
Picha: Mpigapicha Wetu
Mwenyekiti wa Baraza la SUA, Jaji Mkuu Mstaafu Mohamed Chande Othman.

WAHITIMU wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) wametakiwa kuacha kubweteka bali wachape kazi huku wakitumia ujuzi wa taaluma wanazopata kutatua changamoto za kijamii kwenye kilimo na mifugo.

Mwenyekiti wa Baraza la SUA, Jaji Mkuu Mstaafu Mohamed Chande Othman, alisema hayo juzi kwenye mahafali ya 43 ya chuo hicho yaliyohudhurishwa zaidi ya wahitimu 700 na Mkuu wa Chuo, Jaji Joseph Warioba. 

Jaji Chande alisema SUA hufundisha masomo ya sayansi, kilimo na mifugo kwa nadharia na vitendo na kwamba  mhitimu akiitumia vizuri nafasi aliyoipata, itamsaidia kupiga hatua katika kukamilisha kusudia lake la kuisaidia jamii kuinuka katika nyanja zote muhimu zikiwamo kilimo na mifugo. 

Naye Naibu Makamu Mkuu wa SUA anayeshughulikia Taaluma, Utafiti na Ushauri, Prof. Maulid Mwatawala, aliwataka wahitimu kujenga dhana ya kutosubiri kuajiriwa bali wajiajiri na kutumia ubunifu walio nao katika kutatua changamoto mbalimbali nchini. 

Prof. Mwatawala alisema iwapo watatumia ubunifu, watafanikiwa kutoa elimu waliyoipata kwa wahitaji hata kabla ya kupata ajira, kukabiliana na changamoto zilizopo. 

Mmoja wa wahitimu wa chuo hicho, Amina Malongo, aliwashauri wahitimu wenzake kujenga tabia ya kujituma katika utekelezaji wa kazi zao jambo litakalowasadia kufikia malengo ya kilimo. 

Alisema mhitimu kupitia elimu aliyoipata, anaweza kujiajiri na kutatua changamoto zinazowakumba wafugaji na wakulima.  

Pia alisema kwa kutumia elimu wanaliyoipata wana nafasi ya kujiajiri na kujikita katika mambo mbalimbali muhimu yakiwamo ya ufugaji wa samaki, kilimo na kuendeleza ufugaji na kutatua changamoto za kilimo hasa kwa wakulima wadogo. 

Awali, Makamu Mkuu wa SUA, Prof. Raphael Chibunda, alisema chuo kinastahili kujipongeza kwa kuongeza idadi ya nguvu kazi yenye taaluma, ujuzi na weledi kila mwaka ikiwa ni chachu ya kuongeza kasi ya maendeleo nchini.