‘Wakulima Kanda Kati wanazalisha chini ya kiwango’

By Renatha Msungu , Nipashe
Published at 06:56 AM Apr 20 2024
Pichani wakulima wakiwa shambani.
Picha: Maktaba
Pichani wakulima wakiwa shambani.

MWENYEKITI wa Bodi ya Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA), Dk. Anthony Diallo, amesema wakulima wa Kanda ya Kati wanazalisha chini ya kiwango kutokana na dhana potofu waliyonayo ya matumizi ya mbolea kuharibu udongo wa mashamba yao.

Dk. Diallo alisema hayo juzi wakati akizungumza na wadau wa kilimo wa Mkoa wa Singida, ikiwa ni ziara ya wajumbe wa Bodi na Menejimenti ya TFRA iliyolenga kutoa elimu na kuhamasisha matumizi sahihi ya mbolea kwa wakulima.

Alisema, wakulima wengi hawataki kutumia mbolea kwa kudhani kuwa inaharibu udongo wa mashamba yao na kuamini kuwa itasababisha wavune mazao kidogo. 

Dk. Diallo alifafanua kuwa ili wakulima waweze kuzalisha kwa tija na mazao mengi katika eneo dogo ni lazima wahimizwe kutumia mbolea kwa wakati na kwa usahihi na kwa kuzingatia ushauri unaotolewa na wataalam wa kilimo.

Aidha, Dk. Diallo aliwataka Wakurugenzi na Wakuu wa Wilaya kufuatilia taarifa ya afya ya udogo ya maeneo wanayoyasimamia ili wakulima watumie mbolea kulingana na mahitaji ya udongo wanaolima. 

Alisema, taarifa hiyo pia itasaidia wazalishaji kujua aina ya virutubisho vinavyohitajika katika kila eneo la nchi na kuzalisha na kusambaza kiasi cha mbolea kinachotosheleza mahitaji husika.

"Huwezi kutumia mbolea bila kujua afya ya udongo, hivyo wakulima watumie kutokana na afya ya udongo wa mashamba yao," alisema. 

Mkurugenzi Mtendaji wa TFRA, Joel Laurent, alisema mikoa ya Kanda ya Kati na Kanda ya Ziwa imeendelea kuwa na matumizi madogo ya mbolea kutokana na mwamko mdogo na kusababisha wakulima kuzalisha chini ya kiwango.

Alisema ili kuongeza matumizi ya mbolea, aliwataka maofisa ugani kutoa elimu kwa wakulima kuhusu faida za matumizi ya mbolea ili waweze kutumia na kuongeza uzalishaji.

Kadhalika, aliahidi mamlaka hiyo kusimamia zoezi la kufikisha mbolea kwa wakulima kwa wakati ili kuondoa vikwazo vinavyowafanya wakulima kushindwa kutumia kwenye uzalishaji wao. 

Baadhi ya wadau wa kilimo walioshiriki katika kikao hicho wameomba mbolea hizo ziwe zinawafikia kwa wakati ili kuwaepushia kadhia wanayoipata msimu wa kilimo unapofika na pembejeo hiyo kukosekana sokoni.