Wakulima wa miwa kunufaika upanuzi wa kiwanda cha sukari

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 10:35 AM Jun 21 2024
Kiwanda cha Kilombero.
Picha: Mtandao
Kiwanda cha Kilombero.

WAKULIMA wa miwa wanatarajiwa kunufaika na upanuzi wa Kiwanda cha Sukari Kilombero.

Baada ya kukumbwa na changamoto za msimu uliopita zilizosababishwa na mvua kubwa ya El Nino, kiwanda hicho kimechukua hatua kuwatuliza na kuwafariji wakulima kupitia mradi wa upanuzi wa kiwanda cha K4 ambao umefikia asilimia 90.

Ni uwekezaji unaofanywa na kampuni kwa kuonesha imani yake kwa jamii ya wakulima wa ndani, ambao watazalisha asilimia 60 ya miwa inayohitajika katika kiwanda hicho.

Pierre Redinger, Mkurugenzi wa uzalishaji wa kilimo wa kampuni hiyo, alisema jana kuwa katika mashamba ya miwa kuwa, "safari hii ilianza mwaka 2018 kwa usajili wa wakulima, ikiungwa mkono na Ofisi ya Mkuu wa Wilaya, ambayo ilifungua njia kwa biashara hii muhimu."

Redinger pia alitangaza kuwa Kampuni ya Kilombero Sugar imejitolea kutoa mkopo wa mbegu za miwa tani 20,000 kwa wakulima, kwa msimu wa upandaji wa 2024/25 na 2025/26, ambao utasaidia zaidi upanuzi huo.

George Gowelle, Mwakilishi wa Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Sukari Tanzania, alieleza mchango wa serikali katika mradi huo, akisema kuwa serikali itaendelea kuunga mkono juhudi zinazolenga kuongeza utoshelevu wa sukari. 

Alisema, "Kilombero Sugar imeweka mfano wa kuigwa, na serikali itaendelea kuunga mkono jitihada kama hizi." 

Bakari Mkangama, Mwenyekiti wa Kilombero Joint Enterprises Cooperatives Society, inayowakilisha AMCOS 17 zinazofanya kazi moja kwa moja na Kampuni ya Kilombero Sugar, alisifu  hatua hiyo kama fursa ya mabadiliko. 

 "Mpango huu utaleta mabadiliko makubwa kwa soko letu la kuaminika, kipato endelevu na kuboresha maisha. Tunapaswa kuchangamkia fursa hii adhimu," alisema. 

Mgeni Rasmi, Mkuu wa Wilaya ya Kilombero, Dunstan Kyobya, alipongeza juhudi  za Kilombero Sugar, akisema upanuzi wa kiwanda cha  K4 na kampeni ya kuinua wakulima ni jambo muhimu kwa kipato endelevu kitakachoboresha maisha ya wakulima wa miwa katika Bonde la Kilombero.

"Serikali imejitolea kuunda mazingira mazuri kwa uwekezaji wa biashara na ustawi wa jamii," alisema Mkuu wa Wilaya.