Wananchi kukopeshwa bil. 10/- kupitia simu

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 09:04 AM May 27 2024
Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Abdulmajid Nsekela.
Picha: Maktaba
Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Abdulmajid Nsekela.

WANANCHI milioni moja wanatarajiwa kuwezeshwa mikopo ya zaidi ya Sh. bilioni 10 kupitia simu zao.

Hatua hiyo inatokana na Benki ya CRDB kuingia makubaliano na kampuni ya mawasiliano ya Tigo Tanzania kuwezesha wateja wa Tigopesa wanaokidhi vigezo vya kukopa kuanzia Sh. 500,000 mpaka milioni mbili kufanya hivyo kupitia huduma ya Tigo Nivushe iliyoboreshwa.

Akizungumza na waandishi wa habari wakati wa hafla ya kutia saini mkataba huo, Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Abdulmajid Nsekela, alisema makubaliano hayo yanalenga kuwezesha Watanzania kupata mkopo utakaowasaidia kufanikisha shughuli zao mahali popote walipo, hivyo kuchangia kasi ya kukuza kipato cha mwananchi mmoja mmoja na uchumi wa taifa kwa ujumla.

"Benki ya CRDB inatarajia kuhudumia wateja wa Tigo Nivushe wanaokidhi vigezo vya kukuwawezesha kupata mikopo ya kuanzia kuanzia Sh. 500,000 mpaka Sh. milioni mbili. Kwa miaka mitatu ijayo, tunatarajia kuwekeza zaidi ya Sh. bilioni 10 kwa ajili yao na kupata wateja zaidi ya milioni moja,” alisema Nsekela.

Mkataba huo, Nsekela alisema umetiwa saini baada ya kufanya majaribio kwa miezi mitatu na kuwafikia takriban wateja 100,000, hivyo pande zote mbili kujiridhisha kwamba zipo tayari kuanza kuwanufaisha Watanzania wenye uhitaji na fedha kwa matumizi tofauti.

Mkurugenzi huyo alisema wanafahamu ukubwa wa uhitaji wa mikopo nafuu walionao wananchi hasa wale ambao hawatumii huduma za benki, hivyo wanashirikiana na kila mdau anayeweza kusaidia kuwafikia wananchi na kampuni ya Tigo ni miongoni mwa taasisi walizoona ni sahihi kufanikisha lengo hilo.

Kwa sasa, serikali inatekeleza Mpango Mkakati wa Tatu wa Taifa wa Huduma Jumuishi za Fedha wa Mwaka 2023 – 2028 chini ya Baraza la Taifa la Huduma Jumuishi za Fedha ili uendeleza mafanikio yaliyopatikana katika mkakati wa pili ikiwamo ongezeko la watu wazima wanaotumia huduma rasmi za fedha nao wakiongezeka kutoka asilimia 65 mwaka 2017 hadi asilimia 76 mwaka 2023. 

Taarifa ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT0 inasema mafanikio haya yanaelezwa kuchangiwa zaidi na kuongezeka kwa matumizi ya huduma za fedha kwa njia ya kidijitali, uelewa wa huduma za fedha kwa watumiaji, na ushirikiano kati ya wadau wa huduma jumuishi za fedha wa sekta ya umma na binafsi.

Katika Mpango huu wa Tatu, dira ya serikali ni kuona rika la watu wazima na wafanyabiashara wote wanafikiwa na kutumia bidhaa na huduma bora za fedha ili kuboresha ustawi wa maisha yao ya kila siku kwa kuishirikisha binafsi pamoja na wadau wa maendeleo.

Mkurugenzi Mtendaji wa Tigopesa, Angelica Pesha alisema teknolojia imerahisisha kila kitu na idadi ya Watanzania wanaotumia simu za mkononi ambazo ni njia nzuri ya kuwafikishia huduma za fedha inazidi kuongezeka kia siku.

"Takwimu za Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) zinaonesha kuna takriban akaunti milioni 53 za pesa mtandao. Kati ya hizo, akaunti milioni 16.5 ni za Tigopesa. Hawa ni Watanzania waliopo mjini na vijijini, hivyo ushirikiano huu tunaoanza leo na Benki ya CRDB utafika katika kila pembe ya nchi yetu kuwanufaisha wananchi," alisema Angelica.

Katika utoaji huduma kupitia simu za mkononi, Angelica amesema wanao uzoefu wa kutosha, hivyo wanapounganisha nguvu na Benki ye CRDB ambayo ni taasisi kubwa zaidi ya fedha nchini, wanalenga kuacha alama kwa Watanzania wengi ambao sasa hawatopoteza muda wala kutafuta wadhamini kupata mkopo wa mpaka Sh. milioni mbili.

"Huko mtaani kuna masharti mengi ya kukopa Sh. milioni mbili. Utatakiwa uwe na wadhamini pamoja na dhamana lakini sisi Tigo na Benki ya CRDB tumeungana kurahisisha na kuondoa usumbufu huo wote ambapo sasa hivi mtu ataweza kupata fedha anayoihitaji kwenye simu yake," alisema Angelica.