Wananchi wapewa elimu ya fedha kuepuka mikopo umiza

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 09:41 AM May 28 2024
Fedha.
Picha: Mtandaoni
Fedha.

WANANCHI wilayani Bukoba, mkoani Kagera wameshukuru serikali kwa kufikisha huduma ya elimu ya fedha, wakiamini italeta mabadiliko kiuchumi na kuepusha upotevu wa fedha.

Wakizungumza juzi kwa nyakati tofauti baada ya kupata elimu hiyo, wananchi hao, akiwamo mfanyabiashara Ivona Gasper, walisema watawaeleza wenzao kile walichofundishwa ili wawe na uelewa mpana juu ya masuala ya fedha. 

"Tunaiomba serikali iendelee kutoa elimu ya fedha kwa wananchi wake na kuhakikisha inawafikia watu wote nchi nzima kwa sababu wananchi wengi wanapoteza fedha kwa kukosa elimu," alisema Ivona. 

Mwelimishaji Rika Ngazi ya Jamii, Jackline Petro, alisema kuwa baada ya kupata elimu ya fedha, amejua sehemu sahihi ya kutunza fedha zake kama vile benki, vyama vya akiba na mikopo (SACCOS) na vikundi vidogo vilivyosajiliwa. 

Ofisa Usimamizi wa Fedha Idara ya Uendelezaji Sekta ya Fedha katika Wizara ya Fedha, Stanley Kibakaya, alisema serikali itahakikisha watu wote waliokusudiwa kupata elimu awamu ya kwanza wanafikiwa kama ilivyopangwa. 

"Tumejipanga kutoa elimu kwa watu wote, wakiwamo watoahuduma na watumiaji huduma za fedha, ili wawe na uelewa wa pamoja na mambo ya kuzingatiwa kuhusani wakati wa kutoa mikopo au kuchukua mikopo," alisema Kibakaya. 

Ofisa Biashara Mkoa wa Kagera na Mratibu wa Huduma za Fedha Ngazi ya Mkoa, Keneth Mlilo, alisema kumekuwa na mwitikio mkubwa kwa wananchi kujitokeza kupata elimu ya fedha hususan kinamama kwa kuwa imeonekana kundi hilo ndilo waathirika wakubwa wa mikopo umiza yenye riba zisizolipika.