Wasiokuwa na vifaa kuhifadhi taka faini 50,000

By Peter Mkwavila , Nipashe
Published at 06:15 AM Apr 20 2024
Jiji la Dodoma.
Picha: Maktaba
Jiji la Dodoma.

WAFANYABISHARA wanaozalisha taka kwenye maeneo yao jijini Dodoma na wasio kuwa na vifaa vya kuhifadhia uchafu watalazimika kufungiwa biashara zao na kutozwa faini ya Sh. 50,000 hadi 300,000 kwa mujibu wa sheria ndogo za mazingira ya mwaka 2022.

Ofisa Afya wa Jiji la Dodoma, John Lungendo alitoa anagalizo hilo jana jijini hapa alipokuwa akizungumza na wafanyabiashara kutoka sekta mbalimbali baada ya kufanya ziara ya kuwaelimisha umuhimu wa kila mtu kuwa na chombo maalumu cha kuhifadhia taka kwenye eneo lake. 

Akizungumza na wafanyabishara hao wakiwemo wa maduka,machinga,mama na baba lishe,hotelini na wajasirimali, Lugendo alisema watakaokutwa hawana vifaa hivyo jiji litalazimika kufunga biashara zao ikiwa ni pamoja kuwatoza faini hizo kwa mujibu wa sheria.

Alisema, pamoja na kuwaelimisha wafanyabiashara umuhimu wa kuweka vifaa hivyo, jiji halitasita kuwachukulia hatua za kisheria kwa wale watakaokutwa hawajatimiza agizo hilo la uwekaji wa vifaa.

"Jiji pamoja na juhudi kubwa zinazofanywa na watumishi wake wa idara ya afya, watendaji wa kata na mitaa na wadau wa mazingira, bado kuna wakaidi ambao maeneo hawaweki vifaa vya kuhifadhia taka hali inayobabisha kusambaa kwa taka ovyo, sisi kama jiji tutaendelea kuwachukulia hatua za kisheria," alisema.

Pia, aliwataka wafanyabiashara hao kutoka sekta mbalimbali ambao wanazalisha taka kushirikiana na wadau wa mazingira watumishi wa Jiji na vikundi vya kuzoa taka katika kushiriki zoezi la uondoaji wa uchafu ili mazingira yawe safi.

Awali, wakizungumza na waandishi wa habari kwenye uhamasishaji wa vifaa vya kuhifadhi taka, wafanyabiashara hao walisema Jiji la Dodoma bado linakabiliana na changamoto ya ukosefu wa vifaa vya kisasa vya kuzolea taka ikiwamo magari kwenye maeneo mbalimbali. 

"Ili zoezi hilo lifanikishe kuna ulazima wa jiji kuongeza vifaa vyake ambavyo vitakuwa vikifanya kazi kwa muda wote, hii pamoja na kuongeza vikundi vya kuzoa taka pamoja na wafanyakazi kwa upande wa halmashauri hiyo ya Jiji la Dodoma,” alisema. 

Mathias Mtenga, Babalishe anayejishughulisha katika soko la wazi la Machinga, alisema Dodoma hivi sasa uzalishaji taka umeongezeka ni lazima kuwapo kwa vifaa vyakutosha ikiwamo magari, vikundi vya kuzoa na hata kwa wafanyakazi pia.