Wataka Waziri wa Fedha apunguziwe mamlaka, Bunge limulike mikopo yote

By Paul Mabeja , Nipashe
Published at 09:21 AM May 27 2024
Mkurugenzi Mtendaji wa Mtandao wa Madeni na Maendeleo Tanzania (TCDD), Hebron Mwakagenda
Picha: Mtandao
Mkurugenzi Mtendaji wa Mtandao wa Madeni na Maendeleo Tanzania (TCDD), Hebron Mwakagenda

WADAU wa masuala ya madeni na maendeleo wameshauri serikali kushirikisha Bunge kabla ya kukopa ili kuondoa uwezekano wa mikopo kuishia mifukoni mwa watu.

Mkurugenzi Mtendaji wa Mtandao wa Madeni na Maendeleo Tanzania (TCDD), Hebron Mwakagenda, alitoa ushauri huo juzi wakati wa mkutano wa kitaifa wa madeni na maendeleo wenye lengo la kujadili mwenendo wa Deni la Taifa. 

Mwakagenda alisema wanashauri badala ya Waziri wa Fedha kupewa mamlaka ya kukopa kama ilivyo sasa, utaratibu huo ubadilishwe, Bunge liwe na uwezo wa kupitia kila mkopo wa serikali na kujiridhisha kama una tija na taifa. 

"Sisi tunatamani Bunge kushirikishwa kwenye mchakato wa ukopaji mikopo ya serikali badala ya mamlaka hayo kupewa Waziri wa Fedha pekee yake. 

"Kuwapo utaratibu kama serikali inataka kukopa, basi ombi hilo la mkopo kwanza lipitiwe na kamati husika ya Bunge, kwani huko ndiko kwenye uwakilishi wa wananchi, hali hii pia itasaidia kuondoa uwezekano wa mikopo kuishia mifukoni mwa watu," alisema. 

Mwakagenda alisema zipo baadhi ya nchi Afrika ambazo fedha za mikopo zilikopwa na huishia mifukoni mwa watu. 

"Lakini kama Bunge litashirikishwa na kuwa na wataalamu huru ambao watapitia maombi ya mikopo kutoka kwa Waziri wa Fedha basi mikopo itakayokopwa itakwenda kwenye miradi iliyokusudiwa na si vinginevyo. 

"Kamati ya Bunge itakuwa na uwezo wa kumhoji waziri, mkopo ni kwa ajili ya kitu gani na itasaidia kukopa tu pale ambapo kuna uhitaji na ulazima lakini tukikopa lazima tuhakikishe deni linalipwa," alisema. 

Aliongeza kuwa hivi sasa nchi nyingi za Afrika zimeingia kwenye mzigo wa madeni makubwa kutokana na kukopa pasi na kuwajibika. 

Alisema nchi za Afrika zinapaswa kubadilika ili kuondokana na mzigo wa ukuaji Deni la Taifa, hali inayosababisha serikali kutenga kiasi kikubwa cha fedha kuhudumia deni na kusababisha baadhi ya miradi ya maendeleo kushindwa kutekelezwa. 

"Tunapaswa kukopa kwa uwajibikaji, tukope pale tu kwenye ulazima, tukope kwa kuangalia kizazi kijacho kwani tunaweza kukopa leo lakini mzigo tukawaachia watoto wetu.

"Hivi karibuni wakati wa maadhimisho ya miaka mitatu ya Rais Samia Suluhu Hassan, mwenyewe alisema tumekopa sana na kushauri kuwa tupunguze kasi na sisi kama wadau wa masuala haya ya madeni na maendeleo tulifurahia sana kusikia ile kauli," alisema.

Mwakagenda alisema serikali inapaswa kujiimarisha kwenye ukusanyaji mapato ili kuwa na uwezo wa kulipa madeni yote inayokopa badala ya kukopa sehemu ili kulipa sehemu nyingine.

"Wenzetu Uganda uwanja wao wa ndege umechukuliwa kulipa deni, Zambia shirika lao la umeme limechukuliwa kufidia deni, hivyo tujiandae, hizi ndizo athari za kukua kwa Deni la Taifa," alisema Mwakagenda. 

Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) inaonesha katika kipindi cha mwaka 2022/23, Deni la Serikali liliongezeka kwa asilimia 15 na kufikia Sh. trilioni 82.25 huku serikali ikisisitiza kuwa bado ni himilivu.