Watakiwa kutumia fursa kupaa bei ya asali

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 10:14 AM May 28 2024
news
Picha: Mtandaoni.
Asali.

KATIBU Tawala wa Wilaya ya Tabora, Asha Churu, amewataka wananchi mkoani Tabora kutumia fursa ya kupanda kwa bei ya asali ili kujikwamua kiuchumi.

Alitoa ushauri huo juzi alipomwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Paul Chacha wakati wa maadhimisho ya Siku ya Nyuki Dunia.

Alisema kuwa Mkoa wa Tabora hususani Manispaa ya Tabora imejikita katika shughuli za uchakataji mazao ya nyuki na kwamba kuna misitu na maeneo ya kutosha.

Alisema kufanya uwekezaji wa mazao yatokanayo na nyuki yana faida kubwa kwa afya za binadamu pamoja na ukuaji wa uchumi.

"Kwa sasa bei ya asali imezidi kupaa ambapo kilo moja ni Sh.10,000 na kwa Dar es Salaam ni kati ya Sh.15,000 hadi Sh. 20,000 na ikipelekwa nje ya nchi bei inapanda zaidi na kuwezesha mhusika kupata faida kubwa," alisema.

Makamu Mkuu wa Chuo cha Mafunzo ya Ufugaji Nyuki (BTI) mkoani Tabora, Mohamed Wawa, alisema wamejikita kuzalisha wataalamu bora waliobobea ili kuisaidia jamii kufikia malengo ya kuhakikisha zao hilo kuwa juu kibiashara.

Alisema kuwa nyuki anazalisha bidhaa kama asali, nta, gundi, maziwa, supu, sumu na poleni ambazo zote zina kazi yake.

Alisema faida ya asali ni kwa mahitaji ya afya, lishe na tiba ya mwilini na nyingine kuzalisha bidhaa mbalimbali ikiwa ni faida kwa watumiaji na zaidi kuwapatia vipato na kuinua uchumi wa mtu mmoja mmoja na taifa.