Watanzania wahimizwa kuchangamkia fursa sekta madini

By Maulid Mmbaga , Nipashe
Published at 05:21 PM May 20 2024
Katibu Mtendaji wa Tume ya Madini, Mhandisi Yahya Samamba, akizungumza juu ya kufanyika kwa Jukwaa la Tatu la Utekelezaji wa Ushirikishwaji wa Watanzania katika Sekta ya Madini.
Picha: Mpigapicha Wetu.
Katibu Mtendaji wa Tume ya Madini, Mhandisi Yahya Samamba, akizungumza juu ya kufanyika kwa Jukwaa la Tatu la Utekelezaji wa Ushirikishwaji wa Watanzania katika Sekta ya Madini.

WATANZANIA wamehimizwa kuchangamkia fursa za uwekezaji zilizoko katika Sekta ya Madini ili kuchangia katika kuinua uchumi wa taifa kwa kutengeneza ajira na walipa kodi wapya.

Hayo yamesemwa leo Mei 20, 2024 mkoani Dodoma na Katibu Mtendaji wa Tume ya Madini, Mhandisi Yahya Samamba ikiwa bado siku mbili kufanyika kwa Jukwaa la Tatu la Utekelezaji wa Ushirikishwaji wa Watanzania katika Sekta ya Madini ambalo litaanza rasmi Mei 22, mkoani Arusha.

Mhandisi Samamba amesema kuwa, kuna fursa nyingi katika sekta ya madini kutokana na mazingira bora yanayowavutia wawekezaji huku akiwasisitiza watanzania kuchangamkia fursa hizo.

“Watu wajitokeze kwa wingi siku ya jukwaa ili kubaini fursa zilizopo katika sekta hii ya madini na kuzichangamkia,” amesema Mhandisi Samamba.

Ameongeza kuwa jukwaa hilo ambalo mgeni rasmi ni Waziri wa Madini, Anthony Mavunde, litatoa elimu ya kuyafahamu mengi kutoka kwenye sekta ya madini na namna ya kuzifikia fursa zilizopo ili kuchochea zaidi ukuaji na mchango wa sekta hiyo kwenye pato la taifa.

”Sisi tutahakikisha watanzania wanabaini na kuzichangamkia fursa zilizopo, kuyafahamu pia malengo ya serikali ni yapi kwa sababu fursa zipo nyingi lakini zisipotangazwa hakuna atakayezifahamu,” amesema Mhandisi Samamba.