Waziri ataka kasi ukaguzi wa mizani

By Paul Mabeja , Nipashe
Published at 07:54 AM May 25 2024
Waziri wa Biashara na Maendeleo ya Viwanda Zanzibar, Omar Shaaban.
Picha: Mpigapicha Wetu
Waziri wa Biashara na Maendeleo ya Viwanda Zanzibar, Omar Shaaban.

WAZIRI wa Biashara na Maendeleo ya Viwanda Zanzibar, Omar Shaaban, ameitaka Wakala wa Vipimo (WMA) kuongeza kasi ya ukaguzi kwa watu wanaochezea mizani ili kuhakikisha wananchi wanapata bidhaa kwa thamani ya fedha.

Omar aliyasema hayo juzi alipotembelea banda la WMA baada ya kufungua maonyesho ya Wiki ya Viwanda na Biashara yanayofanyika katika viwanja vya Bunge yakiwa na lengo la kutoa elimu kwa wabunge kuhusu majukumu na kazi zinazofanywa na taasisi zilizoko chini ya Wizara ya Viwanda na Biashara.

Alisema  ni muhimu kwa taasisi hiyo kufanya ukaguzi mara kwa mara ili kuwabaini na kuwachukulia hatua kali wafanyabiashara ambao wamekuwa wakiwapunja wanunuzi kwa kuchezea mizani.

Kadhalika, alipongeza WMA kwa kuendeleza ushirikiano na taasisi ya Wakala wa Vipimo Zanzibar (ZAWEMA) na kuahidi kuendelea kutoa ushirikiano kwa taasisi hizo mara kwa mara ili kuhakikisha zinatimiza lengo kuu ambalo ni kumlinda mlaji kupitia matumizi sahihi ya vipimo.

Kaimu Ofisa Mtendaji Mkuu wa WMA, Alban Kihulla, alisema kupitia maonyesho hayo yaliyoandaliwa na Wizara ya Viwanda na Biashara, wabunge mbalimbali wametembelea banda la wakala na kupata ufahamu kwa undani majukumu ya taasisi hiyo hususani katika maeneo ya uhakiki wa dira za maji na alama.

Akitoa elimu kwa wabunge,  Kihulla alisema kwa mujibu wa sheria ya WMA Sura Na. 340 mazao yoye ya shamba yanatakiwa kufungashwa kwa uzito usiozidi kilogramu 100 na endapo gunia litafungashwa kwa uzito zaidi ya ule unaokubalika kisheria, hatua zitachukuliwa dhidi ya msafirishaji na mmiliki wa mzigo.  

Kihulla alisema WMA inaendelea kuwasihi wafanyabiashara na wamiliki wote wa vipimo kuhakikisha vipimo vyao vinakuwa sawa kila mara ili kutenda haki wakati wote bila kuwapunja watumiaji wa huduma katika maeneo yao.