NEMC yapiga kambi Kanda ya Ziwa kuelimisha matumizi ya zebaki

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 10:38 AM May 01 2024
Meneja wa usajili wa kemikali na maabara za kemia, kutoka Ofisi ya Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali Musa Kazumila, akitoa elimu ya matumizi sahihi ya Zebaki kwa wachimbaji wa Wilaya ya Misungwi Mwanza.
Picha: Mpigapicha Wetu
Meneja wa usajili wa kemikali na maabara za kemia, kutoka Ofisi ya Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali Musa Kazumila, akitoa elimu ya matumizi sahihi ya Zebaki kwa wachimbaji wa Wilaya ya Misungwi Mwanza.

BARAZA la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) kwa kushirikiana na ofisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali wameanza kampeni uya kutoa elimu kuhusu matumizi sahihi ya zebaki kwa migodi ya dhahabu kanda ya ziwa.

Akitoa elimu hiyo kwa wachimbaji wa migodi ya Wilaya ya Misungwi Mwanza, Meneja wa usajili wa kemikali na maabara za kemia, kutoka Ofisi ya Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali Musa Kazumila, alisema elimu hiyo inatokana na mataakwa ya mkataba wa Minamata (Minamata convention).

Alisema mkataba huo unataka kutekeleza matakwa yake ambapo moja likiwa la kudhibiti matumizi ya zebaki kwa wachimbaji wadogo na kuongeza kuwa wameanza na wachimbaji wa migodi ya Chata, Shokeraera, Shilalo na luhala zilizopo Wilaya ya Misungwi mkoani Mwanza.

Alisema katika mradi huo unaofadhiliwa na Benki ya  Dunia na  kuratibiwa na (NEMC), Mkemia Mkuu amepewa jukumu la kutoa elimu ya usimamizi salama pamoja na matumizi salama ya zebaki kwani ndiye anayesimamia utekelezaji wa Sheria Na.3 ya mwaka 2003 inayohusu usimamizi na udhibiti wa kemikali za viwandani na majumbani ikiwemo zebaki.

Meneja wa usajili wa kemikali na maabara za kemia, kutoka Ofisi ya Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali Musa Kazumila, akitoa elimu ya matumizi sahihi ya Zebaki kwa wachimbaji wa Wilaya ya Misungwi Mwanza.
Aidha, alisema  lengo la utoaji wa elimu hiyo pia ni kuwajengea uwezo wachimbaji na watumiaji wa zebaki ili waweze kutambua jinsi zebaki inavyoingia mwilini, madhara yake namna ya kujikinga.

Naye Dereki Masako, kutoka Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali Dodoma, aliainisha maeneo ambapo madhara ya zebaki yanatokea kuwa ni wakati wa usagaji wa mawe na kudondosha matope ili zebaki ikamate na wakati wa uchukuaji wa kusanyiko anapokamua na kitambaa kwani matone hudondoka chini na kusambaa ardhini na hewani na kuleta madhara.

Alisema ni vyema wachimbaji wakatumia vifaa Kinga ili kujilinda dhidi ya athari za zebaki na kubainisha madhara yake kuwa ni kuharibu mfumo wa fahamu na kuleta athari ya kushindwa kuhisi, kukakamaa kwa mwili, macho na kuharibika kwa Figo.

Alisema zebaki huathiri ukuaji wa mtoto kwa mama mjamzito kupita kwenye kondo la mama, kupoteza nguvu za kiume kwa wanaume, msongo wa mawazo na mwili kuwasha na kupungua.

Mmoja wa wachimbaji, Haji Nasri, alikiri kutokuwa na uelewa wa madhara ya zebaki na kwamba wamefurahishwa  na elimu hiyo kwani wengi wao wamekuwa wakijishughulisha na uchimbaji wa dhahabu bila kuzingatia madhara ya kiafya yanayoweza kutokea.
Wachimbaji wa dhahabu Misungwi Mwanza wakisikiliza mada kutoka kwa wawezeshaji wa Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) na ofisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali.