Ataka wabunge waonje joto la kikokotoo

By Vitus Audax , Nipashe
Published at 09:58 AM Apr 19 2024
Bla Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
PICHA: MTANDAO
Bla Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

MBUNGE wa Viti Maalam, Kunti Majala, ameliomba bunge kujadili kupitisha kanuni mpya ya kikokotoo cha mafao kwa wastaafu ili ianze kutumika pia kwa wabunge kama wanaona kinafaa kuendelea kutumika kwa watumishi wanaostaafu.

Kunti ametoa rai hiyo bungeni jijini hapa wakati wa uchangiaji wa makadirio ya mapato na matumizi ya Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR-TAMISEMI) mwaka 2024/25.

Amesema kuna haja ya serikali kuthamini mchango wa watumishi wanaolisadia taifa katika kada tofauti kabla na baada ya kustaafu.

“Kama kikokotoo tunakiona ni haki, hebu tuanze sasa tena mwezi wa sita kikokotoo kituhusu tuanze nalo humu ndani mwakani mwezi wa sita kituhusu.”

“Si tunaona haki na ni sawa na hakina shida? Tuanze  na sisi wabunge kutunziwa tupewe kidogo kidogo maana kwa sababu tunapokosa ubunge pia tunakuwa na maisha magumu zaidi hata ya hao watumishi tunaosema tuwatunzie fedha zao,” amesema.

Mbunge huyo pia ameiomba serikali kuona umuhimu wa kutoa motisha kwa walimu na watumishi mbalimbali wanaokwenda kufanya kazi kwenye halmashauri zenye miundombinu isiyo rafiki kupewa motisha ya posho kutokana na kuishi katika mazingira magumu na wakati mwingine kuomba kuhama maeneo hayo.

“Suala lingine ni madai ya watumishi. Watumishi wana hali ngumu pamoja na mambo mengine walionayo kwanini hii stahiki yao wanayodai hatutaki kuwalipa, shida ni nini watu hawa wanadai haki yao wala siyo hisani na kama haiwezekani basi tuambie sameheni mmetoa msaada kanisani msikitini,” amesema.

Naye Mbunge wa Tarime Vijijini (CCM), Mwita Waitara, amemtaka Waziri wa Nchi OR-TAMISEMI, Mohamed Mchengerwa, kutokufumbia macho suala la kikokotoo bali aliwasilishe kwa Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuwa watumishi wa Tanzania zaidi ya asilimia 60 wanahitaji kusikia mabadiliko.

“Watumishi wanahitaji kupata majibu namna tunavyopeleka unafuu katika kikokotoo, Wabunge tumeishasema lipokee kama hoja ya bunge kwa niaba ya watumishi na wastaafu kwani wanahitaji kuona linafanyiwa kazi na kabla ya bunge hili kuisha wapate majibu na kauli ya Rais,” amesema Waitara.